Kumekucha tamasha la Tulia

Muktasari:

  • Tamasha hilo lina lengo la kuenzi utamaduni na mila za watu wa mkoa ya Mbeya na Tanzania kwa ujumla

Rungwe. Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Julius Chalya amewahakikisha usalama wa kutosha wageni na wenyeji katika kipindi chote cha Tamasha la ngoma za asili lijulikanalo kama ‘Tulia Traditional Dances Festival’ lililoanza leo mjini Tukuyu wilayani Rungwe ikihudhuriwa na wageni zaidi ya 2,500 kutoka nje ya Mkoa wa Mbeya.

Chalya amesema Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya imejipanga kuhakikisha usalama kwa wageni wote waliofika mjini Tukuyu kuhudhuria na kushiriki tamasha hilo leo hadi keshokutwa.

“Tumepata wageni wengi watakaohudhuria tamasha kubwa la ngoma ambalo linafanyika kwa mara ya tatu mfululizo wilayani hapa likiwa limeandaliwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

“Kila mwaka kumekuwepo na ongezeko la wageni na mwaka huu inakadiriwa zaidi ya wageni 2500 tayari wamewasili wilayani Rungwe kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, sisi kama wenyeji wa tamasha na wgeni wetu tunawahakikishia usalama kwa muda wote watakaokuwa hapa,” amesema Chalya.

Akizungumzia tamasha hilo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson amesema tayari vikundi vya ngoma 108 kutoka Bara na Zanziba vimeshawasili wilayani Rungwe kwa ajili ya kushiriki tamasha hilo.

“Mwaka huu kumekuwa na ongezezeko za kubwa la watu, lakini na vikundi mwaka huu tumealika hadi vikundi kutoka Zanzibar. Pia mwaka huu kuna banda maalumu kwa ajili kuonyesha vyakula vya asili vya kutoka hapa mkoani kwetu Mbeya.”