Tamu, chungu za Wenger ndani Arsenal

Muktasari:

Mfaransa huyo alisaidia Arsenal kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa bila ya kupoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu

London, England. Arsene Wenger alianza maisha yake England kwenye Uwanja wa Ewood Park dhidi ya Blackburn Rovers Oktoba 12,1996 hatimaye leo Ijumaa ametangaza kustaafu kuifundisha Arsenal.

Wenger aliziteka nyoyo za mashabiki wa Arsenal baada ya kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu England, Kombe la FA mara saba na Ngao ya Jamii mara sita, pamoja na kufanikisha klabu hiyo kuhama kutoka kwenye Uwanja wa Highbury kwenda Emirates mwaka 2006, hayo ni mafanikio yaliyopatikana katika miaka 22 ya Mfaransa huyo.

Wenger mwenye miaka 68, ambaye aliweka rekodi ya kutwaa makombe mawili katika msimu mmoja aliposhinda ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA mwaka 1998 na 2002.

Hata hivyo kwa sasa amewagawa mashabiki wa Arsenal, baada ya klabu hiyo kukaa miaka 14, bila ya ubingwa wa Ligi Kuu, lakini mchango wake katika soka la England umemfanya kuwa mmoja wa makocha wenye rekodi ya kipekee katika soka la sasa.

Wenger msimu wa 2003-04, alikuwa kocha wa kwanza tangu 1888-89 kuiongoza timu kucheza msimu wote bila ya kupoteza mchezo wowote.

Lakini baada ya kutwaa Kombe la FA 2005, ililazimika kusubiri miaka tisa mingine au siku 3,283 kupata taji lingine. Walipata taji hilo baada ya kuifunga Hull City na kutwaa Kombe la FA 2014, kabla ya kutwaa tena taji hilo msimu uliofuata.

Wenger alitwaa taji lake la saba la Kombe la FA msimu uliopita, baada ya kuifunga Chelsea mabao 2-1 kwenye Uwanja Wembley, lakini alimaliza katika Ligi Kuu akiwa nyuma kwa pointi 18 kwa vijana wa Antonio Conte waliotwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Kikosi chake kimekuwa na matokeo yasiyoridhisha katika mashindano ya Ulaya tangu alipocheza fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona mwaka 2006.

Arsenal imetolewa katika hatua 16 bora katika misimu saba mfululizo na msimu wa mwisho kucheza hatua hiyo ya Ligi ya Mabingwa ilikuwa 2017, walipofungwa 10-2 na Bayern Munich.

Mwaka 2006, walifanikiwa kuhamia kwenye Uwanja wa Emirates wenye thamani ya pauni 390milioni wakitokea Highbury.

Gunners imekuwa na rekodi ya kufanya usajili wa gharama ndogo kulinganisha na wapinzani wake. lakini Wenger msimu huu amevunja rekodi ya uhamisho wa klabu hiyio mara mbili.

Alimnunua mshambuliaji Mfaransa Alexandre Lacazette kwa pauni 46.5milioni, pamoja na usajili wa mshambuliaji wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang wa pauni 56milioni aliofanya Januari.

Nani mkurithi Wenger

Kocha wa zamani wa Borussia Dortmund, Thomas Tuchel ameanza kuhusishwa kuchukua jukumu hilo, huku Wenger mwenyewe akisema kiungo wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira anaweza kuwa mrithi wake sahihi.

Tuchel anapewa nafasi kubwa kwa sasa, pia yupo kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Low pamoja na kocha wa zamani Real Madrid, AC Milan na Chelsea, Carlo Ancelotti wametajwa kuwania nafasi hiyo.

Arsenal imesema wanataraji kumtaja mrithi wa Wenger haraka iwezekanavyo.