Ligi Kuu, FDL hatarini

Muktasari:

Kwa sasa klabu za Ligi Kuu zinanufaika na mapa-to ya haki za televisheni kutoka Azam TV na fedha zilizopungua za milangoni. Kampuni ya Vodacom ili-yokuwa ikilipa gharama za usafiri imejiondoa.

Uamuzi wa kuongeza timu za Ligi Kuu kutoka 16 hadi 20 ulionekana kuwa ungeongeza ushindani, kuwapa wachezaji fursa ya kucheza mechi zaidi na kuimarisha timu za Taifa, lakini kuna kila dalili kuwa machungu yake ni makubwa zaidi; yanaweza ama kuivuruga au kuondoa msisimko na utamu.

Uamuzi huo, ambao pia umeinufaisha Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutoa timu zaidi zinazopanda, umekumbana na vizingiti kama kampuni kubwa ya simu ya Vodacom kutoendelea na udhamini na biashara kuyumba na hivyo kampuni kutowekeza katika soka.

Zaidi ya yote umekumbana na utekelezaji wa kanuni inayotaka timu mwenyeji achukue mapato yote ya mlangoni, kitu ambacho utekelezaji wake uliwahi kushindikana.

Na katika mazingira ambayo idadi ya mechi imeongezeka, safari zimeongezeka, mapato kwa klabu yamepungua, hamasa ya mashabiki kufurika viwanjani imepungua na sheria ya kushusha timu itakayoshindwa kuenzi mechi zake ikiwa imesimama, hali ya klabu kiuchumi imezidi kuwa ngumu na lolote laweza kutokea wakati wowote, Mwananchi imebaini.

Tayari wachezaji wameanza kudai mikataba yao na klabu kuvunjwa kutokana na kutolipwa mishahara na stahiki zao nyingine, timu kuzuiwa kutoka hotelini kwa kukosa fedha za pango, timu ya daraja la kwanza kusafiri na wachezaji 13 tu huku sheria inayohalalisha kuvunja mkataba wa mchezaji asipolipwa fedha zake ikiwa imesimama.

Hayo ndiyo yanayotawala habari za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa sasa, achana na habari za utajiri unaohubiriwa wa klabu za Simba, Yanga na Azam.

Kutokana na kadhia ambazo zimeanza kuonekana, kusipokuwa na uangalizi wa karibu kwa mamlaka zinazosimamia, huenda hadithi na historia isiyofurahisha ya ligi hiyo ikajitokeza.

Klabu ya Singida United, ambayo msimu uliopita ilionekana kuwa na mipango kabambe ya kupata wadhamini, sasa inahaha kuzuia wachezaji wake kuondoka kutokana na kutolipwa mishahara.

Ilianza kwa kipa Peter Manyika kuondoka, ikifuatiwa na makocha wasaidizi, Jumanne Challe na Mfaume Athuman kujiondoa kabla ya wachezaji watano kati ya sita kuruhusiwa kuondoka kutokana na ukata klabuni hapo.

African Lyon ilimpoteza mshambuliaji kutoka Ufaransa, Victor Dacosta na kocha Soccoia Lionel kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini mambo kadhaa ambayo yanaiweka Ligi Kuu katika hali hiyo. Kwa sasa klabu za Ligi Kuu zinanufaika na mapato ya haki za televisheni kutoka Azam TV na fedha zilizopungua za milangoni.

Vodacom, ambayo ilikuwa ikilipia gharama za usafiri za timu na waamuzi na iliyoweka jumla ya Sh6.6 bilioni kwa miaka mitano, imejiondoa na hadi sasa si TFF wala Bodi ya Ligi (TPL) iliyotangaza kupata mdhamini.

“Bado tunatafuta wadhamini,” alisema rais wa TFF, Wallace Karia miezi minne iliyopita alipoulizwa na Mwananchi. “Wapo ambao tunaongea nao. Hatujalala, tunafanya kazi na tunaamini tufanikiwa na kuondoa changamoto hii iliyojitokeza.”

Ongezeko la timu kutoka 16 hadi 20 limezidisha machungu ya kiuchumi ya klabu. Timu sasa zinalazimika kucheza mechi nyingi zaidi ya msimu uliopita na hivyo kulazimika kusafiri zaidi.

Wakati zikitakiwa kusafiri zaidi, bado haziwezi kuokota hata senti tano ugenini kutokana na kanuni mpya inayozipa mamlaka hayo timu zinazokuwa nyumbani.

“Msimu uliopita tulipata nauli kutoka kwa wadhamini, sasa kama msimu huu mambo bado itakuwa tofauti,” alisema katibu mkuu wa Singida United, Abraham Simba mwezi Agosti.

“Singida United iko Mwanza, ikitoka Mwanza itakwenda Mbeya. Hii nauli tutaitoa wapi.”

Kanuni zinaeleza timu itakayoshindwa kucheza mechi yake itashushwa madaraja mawili.

Wakati klabu zikikumbana na hali hiyo, bado uamuzi haujafurahisha wengi. Makosa yamekuwa yakionekana dhahiri na mwezi Agosti waamuzi kadhaa walisimamishwa.

Waamuzi waliosimamishwa kupisha uchunguzi ni Godfrey Msakila, Sylvester Mwanga, Nassoro Mwinchui, Abdallah Rashid, Nicholas Makaranga na Ahmada Jamada.

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya timu Ligi Kuu ni lazima TFF ililazimika kuongeza idadi ya waamuzi kuendana na mazingira halisi na hivyo kuchukua ambao hawajakomaa na kupaa uzoefu. Makosa mengi ya waamuzi huvuruga utamu wa ligi.

Wakati mambo yakiwa hivyo Ligi Kuu, klabu za FDL pia zinahaha. FDL inatakiwa zinufaike na mafanikio ya Ligi Kuu ili ijipatie fedha za kumudu gharama za uendeshaji, lakini kupungua kwa msisimko wa Ligi Kuu kutakuwa na athari kwa mambo kama posho za waamuzi na safari zao.

Itaendelea kesho