Ligi Kuu sasa yafikia patamu

Muktasari:

  • Mchezo wa jana ulikuwa wa mwisho kwa Yanga kabla ya kwenda Botswana kuvaana na Township Rollers.

Unaweza kusema vyovyote, Ligi Kuu Bara ndiyo imeanza au Ligi Kuu imefikia patamu baada ya Yanga kuikuta Simba kwa pointi 46, baada ya kuibandua Stand United mabao 3-1.

Yanga imefikia pointi hizo baada ya ushindi huo, kwa mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa muda mrefu, Simba ilikuwa ikiongoza kugi hiyo ikiiacha Yanga kwa pointi nane, lakini sasa imezifikia, lakini Simba inajidai na wastani mzuri wa mabao ya kufunga.

Mashabiki wa Yanga jana walitoka uwanjani kwatu wakishangilia ushindi dhidi ya timu hiyo ambayo iliivimbia Simba kwa kulazimisha sare ya mabao 3-3, katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja huo wiki iliyopita.

Mbali na hilo, ushindi wa Yanga umeongeza presha kwa Simba ambayo haina rekodi nzuri ya kutanua pengo la pointi dhidi ya Yanga inapokuwa imetangulia mbele kwa pointi chache.

Msimu uliopita Simba ilishindwa kudhibiti pengo la pointi tano dhidi ya Yanga licha ya kubaki michezo sita ya ligi lakini ilikosa ubingwa.

Simba ilipoteza pointi tano kati ya michezo sita ikifungwa na Kagera Sugar, ilitoka sare na Toto Africans na kulingana pointi na Yanga mwishoni mwa msimu. Simba ilikosa ubingwa kwa tofauti ya uwiano wa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mchezo wa jana ulikuwa wa mwisho kwa Yanga kabla ya kwenda Botswana keshokutwa kuwavaa Township Rollers katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Machi 17, baada ya Yanga kuchapwa mabao 2-1 katika mchezo wa awali. Yanga ilitarajiwa kusafiri usiku wa kuamkia leo kwenda mjini Gaborone, Botswana.

Katika mchezo wa jana, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, walitumia dakika tano kipindi cha kwanza kufunga mabao mawili ya haraka yaliyowavuruga wachezaji wa Stand United.

Licha ya kuanza mchezo huku kikosi chake kikiwa na mabadiliko kadhaa, Yanga ilikuwa na kiu ya kupata ushindi huo muhimu ambao unawaweka katika nafasi nzuri ya kuwatibulia Simba kwenye mbio za ubingwa msimu huu.

Rafael Daud, Maka Edward, Juma Abdul na Gadiel Michael walianza katika mchezo kuchukua nafasi za Haji Mwinyi, Emmanuel Martin, Hassani Kessy, Pato Ngonyani na Thabani Kamusoko walioanza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar.

Mchezo ulivyokuwa

Yanga ilitakata tangu dakika ya mwanzo ya mchezo na kuipa kazi ya ziada Stand United kucheza kwa tahadhari muda wote wa mchezo.

Ubora huo wa Yanga ulizaa matunda baada ya kupata bao la mapema dakika ya saba lililofungwa na kinda Yusuph Mhilu kwa njia ya krosi ambayo iliokolewa vibaya na beki wa Stand United, Erick Mulilo kabla ya mpira kujaa wavuni.

Stand United ambayo ilianza mchezo na mabeki watano, ilishindwa kuhimili mashambulizi ya Yanga na dakika tano baadaye ilijikuta ikiruhusu bao la pili lililofungwa na Ibrahim Ajibu aliyemalizia kwa ustadi pasi ya Daud.

Juhudi za Stand United kutaka kusawazisha zilizaa matunda baada ya kupata bao dakika ya 84 lililofungwa na Vitalis Mayanga.

Yanga ilipata bao tatu lililofungwa na Obrey Chirwa dakika ya 85. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Zambia amefikisha mabao 12 katika Ligi Kuu.