‘Super-sub’ Giroud kama Solskjaer

Muktasari:

Mfaransa huyo amepoteza namba katika kikosi cha kwanza cha Arsenal ila amekuwa na kasi nzuri ya ufungaji

London, England. Olivier Giroud wa Arsenal anafananishwa na mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa, ameingia katika rekodi hiyo kutokana na rekodi yake ya kufunga mabao muhimu akitokea benchi.

Licha ya kocha Arsene Wenger kumuweka benchi muda mrefu, lakini Giroud amekuwa lulu baada ya kufunga mabao dakika za majeruhi na kuinusuru Arsenal huku ujio wa Mfaransa mwenzake Alexandre Lacazette ukimuengua katika kikosi cha kwanza.

‘Super-sub’ Solskjaer alikuwa hodari wa kupachika mabao, lakini akitokea benchi enzi za Sir Alex Ferguson katika kikosi cha Man United. Nguli huyo alifunga mabao 17 kwa miaka 11 aliyokuwa Old Trafford.

Giroud, juzi usiku alikuwa shujaa wa Arsenal, baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika ya 88 katika mchezo waliotoka sare 1-1 na Southampton ‘Watakatifu’.

Mchezaji huyo amefunga mabao 17 aliyofunga akitokea benchi tangu alipojiunga na Arsenal mwaka 2012. Charlie Austin alitangulia kufunga dakika ya tatu ya mchezo.

Giroud amevunja rekodi ya Javier Hernandez, aliyefunga mabao 14 akitokea benchi alipokuwa Man United, wakati Jermain Defoe na Edin Dzeko wana mabao 13 kila mmoja.

Katika orodha hiyo yumo mchezaji wa zamani wa Chelsea Tore Andre Flo (12), Didier Drogba na Salomon Kalou wenye mabao 11 kila mmoja.

Hata hivyo, Defoe anaongoza kwa idadi ya mabao baada ya kufunga 23 katika klabu tofauti alizowahi kucheza katika Ligi Kuu England.