Macho yote leo kwa Bocco, Kagere, Chama

Muktasari:

  • Simba na Mtibwa Sugar zinapeperusha bendera ya Tanzania katika mataifa tofauti Afrika leo.

Kitwe/Dar. Mabingwa wa Tanzania Bara Simba watakuwa na kibarua kigumu leo watakapoikabili Nkana Red Devil ya Zambia lakini macho na akili za mashabiki wa soka ni kwa fowadi matata ya Simba ikiongozwa na Cletous Chama, John Bocco, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Wachezaji hao ndio wamebeba roho za mashabiki wa Simba wakiwaamini ni mahodari wa kutupia hivyo watataka kuwaona wanafanya nini katika mchezo wa leo.

Wakati Simba ikijiwinda kwa Nkana Ligi ya Mabingwa, wawakilishi wengine wa Tanzaia, Mtibwa Sugar wameapa kushangaza umma watakapoivaa KCCA ya Uganda katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Nkana v Simba

Kikosi cha Simba kimeonekana kina morali ya juu kuelekea katika mchezo huo mgumu ambao mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi.

Simba inahitaji ushindi katika mchezo wa leo ili kutanguliza mguu mmoja mbele ili kutinga hatua ya makundi na kuisogelea rekodi yao waliyoweka mwaka 2003 walipofika hatua hiyo.

Timu hiyo inapambana na Nkana baada ya hatua ya kwanza kuitoa Mbabane Swallows ya Swaziland kwa kuifunga jumla ya mabao 8-1 katika mechi zote mbele wakati Nkana wao waliwaondoa Agosto ya Msumbiji.

Kocha wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems alisema anawaheshimu wapinzani na anajua mechi haitakuwa mechi nyepesi lakini amewafuatilia na anajua atatumia mbinu gani ili kupata ushindi.

Alisema wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri yatakayowarahisishia kazi katika mechi ya marudiano itakayofanyia Dares Salaam kati ya Desemba 22 na 23.

“Tunatambua tunacheza ugenini lakini tumejipanga katika mechi zote mbili ili tupate matokeo mazuri na kusonga katika hatua inayofata, kwani malengo ya timu ni kucheza hatua ya makundi msimu huu.

“Nimewafuatilia vya kutosha Nkana na ninazo taarifa zao nyingi kwa maana hiyo tunaingia katika mechi hii tunafahamu mambo yao mengi, “ alisema Aussems.

Morali kama yote

Kiungo mshambuliaji wa Simba Haruna Niyonzima, amesema morali ya wachezaji katika kambi yao ipo juu kuliko kawaida.

Niyonzima alisema anashangaa jinsi waachezaji wote walivyo na morali kubwa kabla hata ya mechi yenyewe. “Tunafahamu ni mchezo mgumu dhidi ya Nkana, lakini morali hii hapa kambini nadhani itachangia kupambana zaidi na kupata matokeo mazuri, “ alisema.

“Kwa niaba ya wachezaji wenzangu kiu yetu ni kuona timu ina kwani kila mchezaji kiu yake ni kuona tunacheza hatu ya makundi msimu huu.

Simba yaitorosha Nkana

kabla ya Simba kuwasili hapa Kitwe Zambia kikosi cha Nkana Rangers kilikuwa kikiishi hoteli ya Road Porty View ambapo huweka kambi kila wanapocheza mechi lakini ghafla walihama baada ya kuona wpainzani wao wameweka kambi katika hoteli iliyopo karibu nao.

KCCA v Mtibwa Sugar

Mtibwa Sugar nao watakuwa na kibarua chao kwenye Uwanja wa Lugogo, Uganda huku wakiapa kushangaza.

Mchezo huo unaotarajiwa kua makali,kwani kila timu imetamba kushinda na kutanguliza mguu moja hatua itakayofuata.Baada ya mchezo wa leo timu hizo zitarudiana Desemba 22 jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo utakaoichezeshwa na mwamuzi Ali Mohammed Adelaid wa Commoro, Mtibwa Sugar imetamba kucheza soka la kiwango na kuibuka na ushindi ugenini.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila alisema wachezaji wake wote wako vizuri na wanasubiri tu waingie uwanjani kutafuta ushindi na wala hawana hofu na wapinzani wao.

“Tumejiandaa vizuri na tumejipanga kuhakikisha tunashinda mchezo wa leo ili iwe kazi rahisi katika mchezo wa marudiano utakofanyika nyumbani.

“Nimewaambia wachezaji wangu kikubwa ni kupunguza makosa mengi tunayofanya na kuhakikisha kila nafasi tutakayopata tunaitumia vizuri,” alisema Katwila.

5-0

Matokeo yaliyoivusha Mtibwa Sugar dhidi ya Dynamos ya Shelisheli.