Shule ya Kawe A, Tumaini zapewa vifaa vya magongo

Muktasari:

  • Mradi wa KITE umejikita kusaidia maendeleo ya wanafunzi kielimu na kitaaluma kupitia njia ya michezo katika shule nane zilizopo wilaya ya Kinondoni na Temeke

Dar Es Salaam. Chama cha Mchezo wa Magongo nchini [THA] imesema kuwa kukabidhiwa vifaa kwa Shule ya msingi ya Kawe A na shule Tumaini ni moja ya mwendelezo wa mchezo huo katika shule.

Hayo aliyasema Katibu mkuu msaidizi  wa chama cha mchezo wa Magongo nchini, Mnoda Magani, baada  ya Shirika la Ocode kupitia mradi wake wa Elimu kwa wilaya ya Kinondoni na Temeke(KITE), kukabidhi vifaa vya mchezo wa magogo kwa Shule ya Kawe A na Tumaini.

 “Ni jambo jema kwa wafadhiri kusaidia vifaa vya mchezo hivyo hakuna budi ya kulipongeza shiriki hili kwa msaada walioutoa,” alisema Magani.

Baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Mwalimu wa michezo wa shule ya Kawe A, Dismas Msambure alisema kuwepo kwa vifaa hivyo kutasaidia kuzidi kuibua vipaji kwa wanafunzi.

Vifaa vya mchezo wa mpira wa magongo ni ghali sana, hivyo tunashukuru shirika la Ocode kupitia mradi wake wa Kite kwa kutuletea vifaa hivi, naamini vitasaidia kuibua vipaji kwa wanafunzi wetu”

“Tulipatiwa mafunzo na shirika hilo kuhusiana na mchezo wa magongo na tayari hapa shuleni tunaendesha mafunzo kwa wanafunzi  kila Alhamisi ”alisema Msambure

Alisema katika shule nyingi  nchini kuna vipaji lukuki vya mchezo huo lakini changamoto iliyopo ni ukosefu wa vifaa vya mchezo huo pamoja na wanafunzi kushindwa kuandaliwa ili aweze kupenda na kujiunga na na mchezo huo.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Kawe A, Redempta Kysima alisema vifaa vilivyotolewa vitasaidia kuibua vipaji vya wanafunzi katika shule hizo, huku vifaa vya tehema vilivyotolewa na mradi huo vitatumika kwa ajili ya matumizi ya ofisi.

Nao wanafunzi wa shule hizo, walisema kuwepo kwa vifaa hivyo kutasaidia wanafunzi wengi kujiunga katika mchezo huo.

Amina Mohamed wa shule ya Tumaini, alisema kupewa vifaa vya mchezo wa magongo  inaleta hamasa kwa wanafunzi kupenda mchezo huo.

Awali, Meneja wa Mradi wa Kite, Samson Sita alisema vifaa vya Tehama walivyotoa katika shule hizo vitasaidia walimu kutengeneza program mbalimbali za kufundishia pamoja na kuandaa ripoti na mitihani .

“Mradi wa KITE umejikita kusaidia maendeleo ya wanafunzi kielimu na kitaaluma kupitia njia ya michezo katika shule nane zilizopo katika wilaya ya Kinondoni na Temeke na kwamba msaada huu tuliyoutoa  katika shule ya Msingi Kawe A na Tumaini una thamani ya Sh 19milioni,” alisema Sita.