Magwiji watatu wamuweka pabaya Simbu London

Muktasari:

Mbio za marathoni za London zitafanyika Aprili 22.

Dar es Salaam. Kama Alphonce Simbu aliruhusiwa kushiriki mashindano ya marathoni ya London kwa sababu za maslahi yake binafsi, basi mwanariadha huyo nyota anatakiwa kufanya juhudi za ziada kutimiza malengo hayo kutokana na mlima mrefu anaokabiliana nao.

Simba, mshindi wa mbio za marathon za 14 za marathoni jijini Mumbai, ameamua kutoshiriki Mchezo ya Jumuiya ya Madola ili ajaribu bahati yake katika mashindano hayo makubwa ya London.

Lakini Simbu atakutana na upinzani mkali kutoka kwa mshindi wa medali tatu katika Michezo ya Olimpiki, Kenesisa Bekele kutoka Ethiopia, mwanariadha wa Uingereza, Mo Farah na nyota wa Kenya, Eliud Kipchoge.

Bekele, 35, anayeangaliwa na wengi kama mwanariadha gwiji wa mbio ndefu na ambaye anashikilia rekodi za dunia za mbio za mita 5,000 na 10,000, alishika nafasi ya pili kwenye mashindano yaliyuopita ya London na mwaka 2016 alikuwa wa tatu.

Akiwa na matarajio ya kuvunja rekodi yaDennis Kimetto ya saa 2:02.57 kabla ya mashindano ya mwaka jana, Bekele alipata majeraha mguuni na kumaliza akiwa nyuma ya Daniel Wanjiru wa Kenya.

“Nimefurahia kurejea London kwa mara ya tatu mfululizo na ningependa kufanya vizuri zaidi ya mwaka jana na kushinda,” alisema Bekele akikaririwa na africanews.com.

“Kwa mara nyingine (mbio za marathoni za) London zimeleta wanariadha bora wa mbio ndefu duniani kwa hiyo najua haitakuwa rahisi… nimekuwa nikifanya mazoezi kwa bidii nikitarajia kluwa nitawasili London April nikiwa katika hali bora.”

Wanariadha hao watatu--Bekele, Farah na Kipchoge-- kwa pamoja wametwaa medali nane za dhahabu za Olimpiki na medali 12 za dhahabu za michuano ya ubingwa wa dunia.

Mbio za marathoni za London zitafanyika Aprili 22.

Simbu, ambaye alizaliwa mwaka 1992, alishiriki mbio za marathoni za ubingwa wa dunia jijini Beijing, China na pia Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2016 nchini Brazil ambako alishika nafasi ya tano, akitumia saa 2:11.15. Mwaka jana alishinda mbio z marathoni za Mumbai.