Mahakama yaipa pigo lingine TFF

Muktasari:

  • Nkundi ni miongoni mwa wahanga wa adhabu ya kufungiwa maisha kujihusisha na soka chini ya utawala wa Wallace Karia kwenye Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo imetoa amri ya kulizuia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi ya mjumbe wa kamati ya utendaji anayewakilisha kanda ya Lindi na Mtwara uliopangwa kufanyika Februari mwakani.

Uamuzi huo wa kuizua TFF kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo umetangazwa leo na Jaji Kiongozi, Dokta Eliezer Feleshi kufuatia ombi la Wakili anayemuwakilisha mlalamikaji Danstan Nkundi kuiomba Mahakama izuie uchaguzi huo wa nafasi ambayo iliachwa wazi baada ya mlalamikaji huyo kupewa adhabu ya kifungo cha maisha kujihusisha na soka.

Mahakama hiyo ilikubaliana na ombi la Wakili Emmanuel Muga anayemuwakilisha Nkundi aliyeiambia kuwa tayari TFF imetoa tangazo la kufanyika uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo huku kesi ya kutengua maamuzi ya kumfungia mjumbe huyo wa kamati ya utendaji ikiwa bado haijatolewa uamuzi.

Kwa mujibu wa Wakili Muga, mahakama imetoa zuio la uchaguzi huo huku ikipanga Februari 15, 2019 kuwa siku ambayo uamuzi wa kesi ya msingi ya kutengua uamuzi wa kumfungia maisha Nkundi kujihusisha na masuala ya soka utatolewa.

Januari mwaka huu, TFF kupitia kamati yake ya maadili ilitangaza kumfungia Nkundi kujihusisha na soka maisha baada ya kumkuta na hatia ya makosa matatu ya kimaadili.

Makosa hayo matatu yaliyomtia hatiani Nkundi ni kughushi nyaraka, udanganyifu wa mapato na kufanya vitendo vinavyoshusha hadi ya mpira wa miguu nchini.

Uamuzi huo ulipelekea Nkundi afungue kesi Mahakama Kuu akiomba itengue adhabu hiyo kwa madai kuwa ilikuwa kinyume na matakwa ya kikatiba.