Mahakama yatoa siku saba kesi ya vigogo Simba

Muktasari:

  • Agizo hilo limetolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya upande wa Mashtaka kueleza mahakama kuwa wapo katika utatekeleza  wa amri ya mahakama ilitolewa Juni 12, mwaka huu.

Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa siku saba kwa upande wa mashtaka kubadilisha hati ya mashtaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili vigogo wa Klabu ya Simba, akiwemo rais wake, Evans Aveva na Makamu wake.

Agizo hilo limetolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya upande wa Mashtaka kueleza mahakama kuwa wapo katika utatekeleza  wa amri ya mahakama ilitolewa Juni 12, mwaka huu.

Wakati agizo hilo inatolewa jana,  mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Evans Aveva alionekana mahakamani, baada ya kutohudhuria kesi yake kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa Figo.

"Natoa siku  saba kuanzia leo( Jana) kwa upande wa mashtaka mhakikishe mnabadilisha hati ya mashtaka ili kesi ya msingi iendelee" alisema Hakimu Simba.

Washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka kumi likiwemo la kula njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka ikionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.

Itakumbukwa kuwa Juni 12, mwaka huu, Mahakama hiyo, ilitoa siku 10 kwa upande wa Mashtaka kufanya marekebisho katika hati ya mashtaka, kwa kuwaondoa mshtakiwa wa tatu na wanne katika kesi hiyo au kuwakamata, ili kesi ya msingi  iweze kuendelea.

Hata hivyo, Julai 5, mwaka huu, upande wa Mashtaka uliieleza mahakama hiyo, kuwa jalada la vigogo hao lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini(DPP), kwa ajili ya kutekeleza amri iliyotolewa mahakama.

Awali, Wakili wa Takukuru Leonard Swai akisaidia na Dismas Mganyizi, alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na wapo katika utekelezaji wa amri ya mahakama iliyotolewa Juni 12, mwaka huu.

Swai alidai kuwa amri hiyo waliyopewa na mahakama kwa sasa inaekelezwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, hivyo wanaomba wiki moja ili waweze kukamilisha amri hiyo.

" Tunaomba muda mfupi ili tuweze kukamilisha utekelezaji wa amri hii kwa sababu mtu anayetekeleza amri hii ni Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, ambaye amerudi kutoka safarini Moshi, hivyo tunaomba siku saba kuanzia leo, atakuwa amekamilisha" alidai Swai na kuongeza kuwa

" Wakili Kimaro anatakiwa kulipitia upya jalada hili kabla ya kubadilisha mashtaka" aliongeza.

 

Baada ya Swai kueleza hayo, Wakili wa utetezi Nestory Wandiba akisaidia na Nehemia Nkoko alidai uamuzi uliotoleea na mahakama ni jambo jema na kwamba wanaomba utekelezwaji wake uwe wa muda mfupi.

Baada ya kusikiliza hija za pande mbili, Hakimu Simba aliutaka upande wa Mashtaka kukamilisha maelekezo ya mahakama kwa wakati kutokana na Kesi hiyo kuwa ya muda mrefu huku washtakiwa wakiendelea kukaa rumande.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 26, mwaka huu itakapotajwa.

Mbali na Aveva, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni  Zacharia Hanspoppe ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba na mfanyabiashara, Franklin Lauwo, ambao mpaka sasa bado hawajakamatwa.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka kumi likiwemo la kula njama, matumizi mabaya na kughushi nyaraka ikionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.

Wanadiawa, kuwa  Machi 10 na 16, 2016, Aveva na Nyange waliandaa nyaraka za kuhamisha dola za kimarekani 3000,000 kutoka kwenye akaunti ya klabu ya Simba kwenda kwenye akaunti ya Aveva wakijua kuwa wanachofanya ni kosa.