Mambo 3 yambeba refa Simba, Yanga

Muktasari:

  • Mwamuzi Jonesia Rukyaa wa Kagera ambaye ameteuliwa na kuchezesha mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Simba na Yanga anazihukumu timu hizo mara ya tatu katika mechi tofauti.
  • Jonesia alichezesha mechi ya kirafiki ya Nani Mtani Jembe baina ya timu hizo Desemba 21, 2013 ambao timu hiyo ilishinda mabao 2-0, Ligi Kuu Februari 20, 2016 Simba ilichapwa 2-0.

Dar es Salaam. Wakati nyota wa Simba na Yanga wakilazimika kuonyesha nidhamu ya hali ya juu ili kukwepa kadi nyekundu za mwamuzi Jonesia Rukyaa, kuna sababu tatu kuu za mwamuzi huyo kuchaguliwa kuchezesha mechi baina ya timu hizo, Septemba 30 jijini zimeanikwa.

Muda mfupi baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumtangaza Jonesia kuwa mwamuzi wa mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama ameainisha vigezo vitatu vya msingi ambavyo viliishawishi kamati yake kumpanga Jonesia badala ya mwamuzi mwingine.

Mwamuzi huyo ambaye Alhamisi iliyopita, Septemba 20 alichezesha mchezo ambao Simba ilichapwa bao 1-0 na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, baada ya raundi moja tu ya ligi kupita, amepewa jukumu zito la kuichezesha tena timu hiyo, safari hii ikiwa ni dhidi ya watani wao wa jadi Yanga.

“Mwamuzi wa kati atakuwa Jonesia Rukyaa kutoka Kagera na atakuwa anasaidiwa na Ferdinand Chacha kutoka Mwanza na mwamuzi msaidizi namba mbili, Mohammed Mkono kutoka Tanga wakati refa wa mezani atakuwa Hery Sasii wa Dar es Salaam wakati huo mtathmini wa waamuzi atakuwa ni Soud Abdi kutoka Arusha na Kamishina wa mchezo atakuwa George Komba wa Dodoma,” alisema Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo.

Akizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya Jonesia kutangazwa, Chama alifichua sababu tatu za msingi zilizochangia mwamuzi huyo kupewa mechi ya watani.

“Kigezo cha kwanza Jonesia ni mwamuzi wa Kimataifa mwenye Beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), pili amefanya vizuri kwenye mitihani na mazoezi ya utimamu kupima ubora na ufanisi wa marefa na tatu ameteuliwa kuchezesha fainali za dunia za wanawake.

Kwa vigezo hivyo hatukuona sababu ya kutomchagua ingawa tuna kundi kubwa la waamuzi bora na wanaofahamu vyema kuzitafsiri Sheria 17 za mchezo wa soka,” alisema Chama.

Huu utakuwa ni mchezo wa tatu wa Simba na Yanga Jonesia amewahi kuchezesha kwa kuwa kabla ya hapo alichezesha mechi ya kirafiki ya Kombe la Mtani Jembe baina ya timu hizo, Desemba 21, 2013 ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mchezo wa pili wa watani wa jadi ambao Jonesia alichezesha ni Ligi Kuu, Februari 20, 2016 ambao Simba ilichezea kichapo cha mabao 2-0.

Uteuzi wake wa kuchezesha mechi hizo, unawalazimisha nyota wa timu zote mbili kucheza kwa nidhamu kubwa na umakini wa hali ya juu ili kujiepusha na kadi ambazo amekuwa akizimwaga kama njugu pale wachezaji wanapoonyesha utovu wa nidhamu.

Rekodi zinaonyesha mechi zote mbili za Simba na Yanga ambazo Jonesia alichezesha, zilimalizika huku timu moja ikiwa pungufu baada ya kutoa kadi nyekundu kutokana na faulo zilizochezwa na mchezaji husika.

Mwathirika wa kwanza alikuwa nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani ambaye katika mechi ya Mtani Jembe alilimwa kadi nyekundu kwa kumchezea madhambi mshambuliaji Ramadhani Singano ‘Messi’.

Pia alipochezesha mara ya pili katika mechi ya Ligi Kuu mwaka 2016, aliyekuwa beki Abdi Banda wa Simba alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea madhambi Donald Ngoma. Banda anacheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini.