Mambo matano moto atakayewania urais Simba

Muktasari:

  • Simba inaingia jijini Mwanza leo sawa na Mtibwa ambao waliondoka juzi Morogoro na tayari wako kwenye viunga vya Mwanza kwa mchezo huo.

Dar es Salaam. Macho na masikio ya mashabiki wa soka wa Simba kwa sasa yako Mwanza kwa mchezo wa kukata utepe wa Ligi Kuu kesho dhidi ya Mtibwa Sugar.

Simba inaingia jijini Mwanza leo sawa na Mtibwa ambao waliondoka juzi Morogoro na tayari wako kwenye viunga vya Mwanza kwa mchezo huo.

Kila mmoja anataka kuona Simba ya Uturuki imejipangaje? Kocha wake Patrick Aussems anajaribu kutuliza mizuka mashabiki wa Simba na kuahidi ushindi huku kocha wa Mtibwa Sugar, Zubeir Katwila naye akijinasibu kwa kusema Simba haitishi wala nini na wataibuka na ushindi katika mchezo huo.

Hiyo siyo ishu sana. Habari kubwa hapa ni suala la uchaguzi wa Simba ambao umebakiza mwezi mmoja na nusu kabla ya muda ambao klabu imepewa kufanya uchaguzi wake mkuu.

Mwananchi limeangalizi changamoto mbili kubwa zinazomsubiri rais ajaye wa Simba. Iko hivi. Julai 24 mwaka huu, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) liliipa Simba siku 75 kuhakikisha inafanya Uchaguzi Mkuu baada ya uongozi uliopo madarakani kumaliza muda wake na sasa zimebakia takribani siku 50.

Simba imeanza kutekeleza agizo hilo kwa kuunda na kutangaza kamati ya watu watano kwa ajili ya kuratibu, kusimamia na kuendesha mchakato wa uchaguzi.

Kamati hiyo ambayo ilitangazwa Agosti 12, iko chini ya mwenyekiti Boniface Lyamwike, makamu mwenyekiti akiwa Wakili Steven Ally, wajumbe ni Issa Batenga, Iddy Mbita na Richard Mwilaba.

Hata hivyo wakati kamati hiyo ikiwa kwenye maandalizi ya kuhakikisha mchakato huo unaanza haraka, mitihani mitano mikubwa inaonekana kumsubiri rais ajaye wa klabu hiyo.

Kwanza ni presha ya mafanikio kwa timu hiyo kwenye Ligi Kuu na mashindano mengine ya ndani na yale ya Afrika na kuhakikisha Simba haifanyi tena makosa kama ilivyokuwa ikifanya vibaya katika kipindi cha takribani misimu mitano mfululizo iliyopita.

Pili ni mchakato wa ujenzi wa uwanja, hosteli na miundombinu mingine, kwani kwa miaka kadha Simba imeendelea kutamba kuwa na eneo kubwa Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, inakotaka kujenga uwanja na hosteli.

Hata hivyo, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘TryAgain’ alisema jana kuwa mkakati wa sasa ni kuitengeneza Simba kuwa ya kisasa zaidi na hata watakaoingia madarakani ionekane kweli Simba imejipanga kwa kutekeleza kila kilicho katika hitaji la Simba.

Wakati wa Tamasha la Simba Day, TryAgain aliwahi kusema kuwa baada ya kumalizika kwa tamasha hilo, kitakachofuata ni kuelekeza nguvu kwenye uwanja wake wa Bunju na zaidi kuhakikisha Simba inakuwa na uwanja kwa ajili ya mazoezi na baadaye uwanja wake wa mechi za kitaifa na kimataifa.

Changamoto ya tatu ni suala la muundo wa klabu. Ikiwa chini ya bodi ya Bodi ya Wakurugenzi, kutengeneza timu yenye ushindani na kuwa kiunganishi kati ya bodi na wanachama kupitia kamati mbalimbali zitakazundwa kuendesha klabu.

Suala la nne ni uwekezaji katika klabu ya Simba. Klabu hiyo inatakiwa kusimamiwa mali zake kwa ukamilifu ikiwemo uwekezaji na ukodishwaji kwa manufaa ya klabu hiyo.

Tano ni ujenzi wa timu za vijana kwa umri mbalimbali ikiwa ni pamoja na timu za wanawake, ngumi na michezo mingine.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya kuratibu mchakato wa mabadiliko, Mulamu Nghambi alisema Simba sio tu inahitaji Rais bali pia wajumbe sahihi ambao wataivusha kutoka hapa ilipo.

“Hatuangalii rais tu, tunahitaji wajumbe sahihi watakaokuwa na maono chanya yatakaoifanya Simba itimize malengo iliyojiwekea.

“Wasidhani kwamba kazi iliyo mbele yao ni nyepesi kwa sababu wanakwenda kuisimamia klabu kupitia bodi “Ni lazima tupate aina ya watu ambao watahakikisha wanafanya kazi kubwa ya kuandaa mikakati madhubuti kama vile kusaka wadhamini pamoja na kutanua vyanzo vya mapato ya klabu.

“Kama inavyofahamika kuwa yale mambo ya Kamati ya Utendaji hayatakuwepo tena hivyo ni lazima wajumbe wa bodi watakaochaguliwa wawe ni watu ambao wana mtazamo wa pamoja wa kuhakikisha Simba inapata mafanikio ya nje na ndani ya uwanja,” alisema Nghambi.