Man City yenye majeruhi kukamilisha ratiba leo

Muktasari:

  • Timu ya Manchester City leo inaikaribisha Hoffenheim ya Ujerumani katika mechi ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi huku ikiandamwa na idadi kubwa ya majeruhi katika kikosi chake cha kwanza.

Manchester England. Timu ya Manchester City leo itakuwa kwenye Uwanja wake wa Etihad kuikaribisha     Hoffenheim ya Ujerumani katika mechi ya mwisho ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo timu hiyo inakabiliwa na idadi kubwa ya majeruhi katika kikosi chake baada ya kiungo David Silva kuumia katika mchezo dhidi ya Chelsea mwishoni mwa wiki iliyopita waliopoteza kwa mabao 2-0 na madaktari wamesema atakaa nje kwa muda.

Kuumia kwake kunamfanya kocha Pep Guardiola kuanza kuchanganyikiwa kwani idadi ya majeruhi imeongezeka huku Ligi Kuu England ikielekea kwenye kipindi kigumu cha mechi nyingi za mfululizo.

Silva amecheza mechi 14 kati ya 16 ilizocheza Man City katika Ligi Kuu England na amecheza mechi zote tano za Ligi ya Mabingwa akiwa na mchango muhimu.

Baada ya mchezo wa leo, Man City itakabiliwa na mechi nne za Ligi Kuu dhidi ya Everton, Crystal Palace, Leicester City na Southampton pia itasafiri kuifuata Leicester kucheza mechi ya robo fainali ya Kombe la Ligi ‘Carabao Cup’ Desemba 18 mwaka huu.

Silva anaungana na majeruhi wengine wa kikosi hicho ambao ni Claudio Bravo, Danilo, Benjamin Mendy, Kevin de Bruyne na shujaa wao wa mabao Sergio Aguero, ambaye Guardiola amepanga kucheza kamari kwa kumchezesha Aguero Jumamosi hii dhidi ya Everton.

Matokeo ya mechi ya leo kwa Man City hayatakuwa na athari yoyote, isipokuwa Hoffenheim inayoburuza mkia katika kundi F ndiyo yenye shinikizo la kushinda huku ikiombea Shakhtar yenye pointi tano itakayoialika Lyon ipoteze mchezo huo ili yenyewe ifikishe pointi sita na kutinga Europa Ligi.

Man City yenye pointi kumi imefuzu hatua ya makundi kwani matokeo ya aina yoyote baina ya Shakhtar na Lyon hayawezi kuiondolea nafasi hiyo isipokuwa yataipata timu itakayoungana nayo.

Lyon yenye pointi saba na Shakhtar yenye pointi tano yeyote itakayoshinda itaungana na Man City kutinga hatua ya 16 bora kutoka kundi F na kuna uwezekano itakayoshindwa ikaangukia Europa Ligi kwani sio rahisi kwa Hoffenheim kupata pointi tatu nyumbani kwa Man City.

Mechi nyingine za leo katika Ligi hiyo zitaikutanisha Valencia vs Man United, Real Madrid vs CSKA Moscow, Viktoria Plzen vs AS Roma, Ajax vs Bayern Munich, Benfica vs AEK Athens,  Shakhtar Donetsk vs Lyon na Young Boys vs Juventus.