Manchester City kwa Arsenal, Man United na Leicester City

Muktasari:

Mabingwa hao wa Ligi Kuu wamepata ratiba nyepesi baada ya kuvaana na Arsenal, watakapovaana na timu tatu zilizopanda daraja msimu huu.

London. Mabingwa wa soka wa England, Manchester City wataanza kutetea taji lao msimu ujao kwa kuvaana na Arsenal ugenini mwishoni mwa wiki ya kuanzia Agosti 11-12.

 

Ratiba ya Ligi Kuu ya England iliyotangazwa leo Alhamisi kwa ajili ya msimu ujao inaonyesha kuwa mechi hiyo pia itakuwa ya kwanza kwa kocha mpya wa Arsenal, Unai Emery katika ligi ya England.

 

Tarehe halisi ya mechi hiyo itathibitishwa wakati ratiba ya televisheni ya kurusha moja kwa moja mechi hizo itakapokuwa tayari.

 

City ilikusanya jumla ya pointi 100 na kufunga mabao 106 na hivyo kumaliza ligi ikiwa juu ya jirani zao wa Manchester United kwa tofauti ya pointi 19 msimu wa mwaka 2017/18.

 

Baada ya mechi ya Arsenal, City haitakutana na timu nyingine zilizoshika nafasi sita za juu hadi Oktoba itakapokwenda ugenini kucheza na Liverpool ambayo iliiondoa timu hiyo inayofundishwa na Pep Guardiola katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu uliopita.

 

Katikati ya kipindi hicho, City itacheza na timu tatu zilizopanda daraja msimu huu za Wolverhampton Wanderers, Cardiff City na Fulham pamoja na timu zilizopanda daraja msimu uliopita za Huddersfield, Newcastle na Brighton.

 

Manchester United itaanza kampeni zake nyumbani kwa kuikaribisha Leicester City na itakuwa na mechi ngumu dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye Uwanja wa Old Trafford.

 

Vijana hao wa Jose Mourinho watavaana pia na Brighton and Hove Albion, Burnley, Watford na Wolves katika mechi nyingine za mwanzoni mwa msimu.

 

Liverpool, iliyofungwa na Real Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya inaonekana kuwa na mechi ngumu mwanzoni mwa msimu kulinganisha na wapinzani wake katika kinyang'anyiro cha ubingwa.

 

Wataanza nyumbani kwa kuvaana na West Ham kabla ya kukutana na Crystal Palace, Brighton na Leicester.

 

Tottenham bado haijaamua kama msimu ujao itacheza mechi zake za nyumbani kwenye uwanja wa Wembley.

Spurs ililazimika kusafiri hadi kwenye uwanja huo wa taifa msimu uliopita wakati uwanja wake wa White Hart Lane ukijengwa.

 

Kazi hiyo bado haijakamilika huku ratiba ikionyesha itaanzia ugenini kwa kuvaana na Newcastle.  

 

Arsenal itakuwa na mwanzo mgumu chini ya kocha Emery, ambaye ana kazi ngumu ya kurithi mikoba ya Arsene Wenger ambaye ameitumikia klabu hiyo kwa muda mrefu, akivaana na Chelsea baada ya mechi dhidi ya Manchester City.

 

Chelsea itaanza kampeni yake kwa kuvaana na Huddersfield na baada ya kukutana na Arsenal itavaana na Newcastle, Bournemouth, Cardiff, West Ham, Liverpool na Southampton.

 

AFP