VIDEO: Manchester United yamtimua Mourinho

Muktasari:

  • Uamuzi wa Man United kumtimua Kocha Mourinho utawagharimu kiasi cha pauni 22 milioni (Zaidi ya Sh46 bilioni) ikiwa ni fidia ya kuvunja mkataba

London, England. Manchester United imemtimua Kocha Jose Mourinho baada ya kuwa na msimu mbaya katika timu hiyo.

Taarifa ya klabu hiyo iliyochapishwa kwenye tovuti yake imesomeka kuwa, “Manchester United inatangaza kuwa imevunja mkataba na kocha Jose Mourinho”.

“Klabu ingependa kumshukuru Jose kwa kazi yake nzuri katika kipindi chote alichokuwa na Manchester United na tunamtakia maisha mema huko aendako.”

Mreno huyo mwenye umri wa miaka 55 katika kikosi cha Manchester United amefanikiwa kutwaa taji la Kombe la Ligi na Ligi ya Europa katika miaka miwili na nusu aliyokaa ndani ya timu hiyo.

Lakini kwa sasa Man United iko katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa nyuma kwa pointi 19 dhidi ya vinara Liverpool ambao waliwafunga mashetani hao wekundu kwa mabao 3-1.

"Kocha atakayechukua jukumu hilo kwa muda anategemewa kutangazwa hivi karibuni, huku tukiendelea na utaratibu wa kusaka kocha mpya," imesema taarifa ya Man United.

Manchester United ilinyanyaswa na kudhalilika ilipocheza dhidi ya Liverpool juzi Jumapili.

Katika mchezo huo, United ilichapwa mabao 3-1 ndani ya dimba la Anfield - mabao mawili yakiwa ya staa wa kimataifa wa Uswisi, Xherdan Shaqiri na moja la Sadio Mane huku bao lake likifungwa na Jesse Lingard.

Katika pambano hilo, Liverpool ilipiga mashuti 36 katika lango la United huku mashetani hao wakifanya majaribio matano langoni mwa Liverpool.

Bao la tatu la Shaqiri lilimaanisha United ilikuwa imefungwa mabao 29 katika mechi 17 wakati katika msimu mzima uliopita ilifungwa mabao 28.

Tofauti ya pointi 19 baina ya Manchester United na Liverpool baada ya mechi 17 haijawahi kutokea katika historia ya klabu hizo mbili.

 

Pia mashetani hao wapo nyuma ya Chelsea inayoshika nafasi ya nne kwa pointi 11 na wachambuzi wawili wanaoaminika katika soka la Uingereza, Jamie Carragher na Gary Neville walikuwa wanataka kocha huyo aondoke.

Carragher anaamini kuondoka kwa Mourinho ni njia pekee ya kuiokoa Manchester United wakati Neville ameilaumu bodi ya timu hiyo kumuongezea mkataba Mourinho wakati wakijua msimu wa tatu huwa unamsumbua kocha huyo.

“Nadhani uamuzi mkubwa kwa Manchester United ni pale patakapokuwa na mabadiliko ya kocha. Iwe kabla ya mwisho wa msimu au mwishoni mwa msimu,” alisema Carragher, beki wa zamani wa Liverpool.

“Baada ya kuitazama timu siyo leo tu (Jumapili iliyopita), bali msimu mzima nimejiuliza hii timu inaweza kweli kushinda ligi? Hapana. Hii ni timu ambayo inapaswa kuwa ya sita katika ligi? Hapana. Siamini kama kuna pengo kubwa la ubora kati ya Liverpool na United.”

 

Amesema, “Nadhani Liverpool ilipambana Zaidi (dhidi ya Man Uniteda). Hata hivyo, msimu huu siamini kama pengo linapaswa kubaki kuwa kubwa sana kama lilivyo sasa.”

“Mourinho anapata ubora wa wachezaji wake? Hapana na wala hakaribii na huyu ni kocha wa kiwango cha juu. Mzunguko wake kama kocha mara zote unakuwa miaka miwili au mitatu. Anafanya makubwa miezi 18 ya kwanza baada ya hapo anachoka.”

Wakati Carragher akisema hayo, Neville anailaumu bodi ya Manchester United kwa jinsi inavyoendesha mambo yake na alikuwa akiamini kocha huyo atafukuzwa msimu huu.

“Mourinho ataondoka? Nadhani itatokea, chaguo langu lilikuwa aende mpaka mwisho wa msimu. Hata hivyo, bodi haijiamini na inashangaza sana. Kumpa mkataba mpya wakati ikijua mwisho wa Mourinho katika makali yake unakuwa miaka mitatu. Mwaka wa tatu siku zote ni mgumu kwake,” alisema Neville.

“Miezi 18 ya kwanza, United ilikuwa ya pili katika ligi ikitwaa mataji mawili katika msimu wake wa kwanza, hiyo ndiyo ingekuwa sababu ya bodi kuendelea kumfanya awe na njaa zaidi katika msimu wake wa tatu. Aliporudi tu katika maandalizi ya msimu mpya alichukiza na klabu ikashindwa kumudu hilo jambo.”

Nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane alidai kuna wachezaji ambao hawana ubora wa kuichezea timu hiyo kwa sasa.

“Nadhani kuna baadhi ya wachezaji wa United si wazuri. Wako mbali kutoka kwa (wale wa Manchester) City na Liverpool. Katika ulinzi wanahitaji msingi bora. Leo (juzi) walikuwa kila mahala. Walionekana wazi wako ovyo na hiyo inatia wasiwasi kwa siku za baadaye,” alisema.

 

“Wachezaji wote hawa wanajaribu kadri wanavyoweza, wanajaribu sana. Lakini (Ander) Herrera anafanya kazi yake vyema, uamuzi mbovu unagharimu mechi.”