Manji aibua mapya Yanga

Muktasari:

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),  Ally Mchungahela, amesema nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga iko wazi na inatakiwa kugombewa katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Januari 13, mwakani.

Dar es Salaam.Uamuzi wa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kurejea katika nafasi yake, umezidi kuchochea vita iliyopo baina ya klabu hiyo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Tofauti na mawazo ya vigogo wa Baraza la Wadhamini wa Klabu hiyo wakiamini kurejea Manji kungerudisha amani na utulivu ulioonekana kuanza kupotea ndani ya klabu hiyo, hali imeanza kuwa tofauti na endapo busara haitatumika, huenda mambo yakawa mabaya.

Kitendo cha kila upande kushikilia msimamo baada ya tamko la Baraza la Wadhamini la Yanga lililotolewa Dar es Salaam juzi, kimeanza kuashiria hatari inayonyemelea uhusiano baina ya klabu hiyo kongwe na TFF.

Ushauri wa Baraza la Wadhamini wa Yanga uliotaka Kamati ya Utendaji ya Klabu hiyo kukutana na Kamati ya uchaguzi ya TFF, umeonekana kuwa kazi bure baada ya upande wa pili kusisitiza hauko tayari kubadili utaratibu uliowekwa katika usimamizi wa uchaguzi wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Januari 13, mwakani.

"Tumewaita kamati ya utendaji wametujibu kuwa kamati ya uchaguzi wanayo. Hata kama isingekuwepo, kamati ya utendaji ilipaswa kuchagua kamati ya uchaguzi kwasababu, uchaguzi kusimamiwa na watu wa nje ni kuvunja Katiba ya Yanga.

“Lakini pamoja na hilo, tunaishauri Kamati ya Utendaji ya Yanga ikutane na Kamati ya Uchaguzi ya TFF wajadiliane na kulipatia suluhu suala hili," alishauri Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Waziri na Kapteni Mstaafu George Mkuchika, juzi alipozungumza na vyombo vya habari.

Mkuchika ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, alitoa tamko hilo juzi, Dar es Salaam aliposoma barua ya Manji ya kukubali kurejea katika nafasi yake ya uenyeketi baada ya kukaa nje kwa siku 538 tangu Mei 23, 2017 alipotangaza kujizulu.

Hata hivyo, TFF kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili Ally Mchungahela umepingana na tamko la Mkuchika na kusisitiza nafasi zote za uchaguzi wa Yanga lazima zijazwe ikiwemo ya mwenyekiti.

"Uchaguzi Mkuu wa Yanga utafanyika kama ulivyopangwa na hakuna chochote kilichobadilika na utaratibu uleule ambao tuliutangaza tutaendelea nao, kimsingi tayari kuna wanachama wengi wameshachukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo ya mwenyekiti.

“Kama Yanga wanamtaka arudi,wakamchukulie fomu, agombee wamchague. Lakini hadi sasa, sisi hatutambui kurejea kwa Manji na mchakato wa uchaguzi uko pale pale. Nafasi zote zilizo wazi zitagombewa ikiwemo ya Mwenyekiti," alisisitiza Wakili Ally Mchungahela.

Tamko la Wakili Mchungahela limekolezwa na kauli ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambalo limesema TFF imepewa baraka zote na baraza hilo kuhakikisha Yanga inafanya uchaguzi mkuu wa kupata viongozi wa kuziba nafasi zilizo wazi ikiwemo ya mwenyekiti.

"Sisi tunashughulika na watu tuliowapa kazi. Taarifa za Yanga zitapelekwa TFF, hivyo ni suala la Yanga kufanya mawasiliano na TFF kwa kufuata taratibu," alisema Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Alex Nkenyenge.

Wakati TFF na BMT zikitoa matamko hayo, Yanga kupitia kwa  Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Matawi, Bakili Makele imesisitiza kuwa haijakataa kufanya uchaguzi kama ambavyo Serikali na TFF imewataka, lakini siyo kwenye nafasi ya mwenyekiti.

"Hatupingi uchaguzi, lakini kila jambo linafuata taratibu. mwenyekiti wetu yupo na sisi wanachama tunamtambua. Na tayari anashirikiana na viongozi wengine katika usajili wa dirisha dogo na amesema Januari 15 atakuwa ofisini rasmi, sasa tufanye uchaguzi wa mwenyekiti wa nini," alihoji Makele.

Matamko hayo yanayoashiria mgongano baina ya Yanga, TFF na BMT, imewaamsha wadau wa klabu hiyo ambao wametoa maoni li kupatikana suluhisho la kudumu baina ya pande hizo zinazokinzana.

"Tufuate taratibu za nchi na klabu. Tuungane kwa maslahi ya klabu na siyo kwa ajili ya mtu, tuwe watulivu na busara itumike katika kumaliza mvutano uliopo, alisema aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadick.

Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars na mchambuzi wa soka, Ally Mayay, aliwataka wanachama wa klabu hiyo kuwa na subira katika kipindi hiki.

"Siku zote wanachama ndiyo wana uamuzi na klabu yao, tayari bodi ya wadhamini imetangaza mwenyekiti yupo, vilevile mkutano mkuu hawakuridhia mwenyekiti kujiuzulu, hivyo ni vema TFF ikakutana na bodi wakubaliane," alisema Mayay.

Pia alisema Yanga inaweza kumchukulia fomu Manji hata kama hatakwenda katika kampeni, lakini nafasi ya kushinda ipo kwa kuwa wanachama wanasema wanamtaka, wafuate utaratibu wa nchi.