Manji aipa Yanga ushindi wa kwanza

Muktasari:

  • Achana na ushindi huo wa mabao 2-1 iliyopata Yanga dhidi ya USM Alger ya Algeria, kitakachowapa raha Wana Jangwani ni maneno matatu aliyoyatoa bilionea huyo kabla ya pambano hilo la Kundi D la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

MASHABIKI na Wanachama wa Yanga wana kila sababu ya kutabasamu baada ya Mwenyekiti wao, Yusuf Manji kuwaibukia ghafla Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, jana Jumapili kisha timu yao ikapata ushindi wa kwanza katika michuano ya CAF.

Achana na ushindi huo wa mabao 2-1 iliyopata Yanga dhidi ya USM Alger ya Algeria, kitakachowapa raha Wana Jangwani ni maneno matatu aliyoyatoa bilionea huyo kabla ya pambano hilo la Kundi D la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Manji, aliyefika uwanjani mapema jana jioni kuwaangaliai vijana wake wakiwajibika dhidi ya USM Alger katika mechi za kukamilisha ratiba za michuano hiyo, amewaambia mashabiki kuwa, watulie kwa kuwa mambo mazuri yanakuja Jangwani.

Akizungumza kwenye chumba maalumu akiwa na baadhi ya viongozi wa Yanga, Manji alisema alikwenda uwanjani hapo kuiangalia Yanga yake na kwamba, kuna mambo mazuri yanakuja na akafichua kuwa atatoa msimamo kuhusu hatima ya kurejea kwake klabuni hapo.

“Nimekuja kuiangalia Yanga yangu, ni muda mrefu na pia nataka kuwaambia Wanayanga kuwa, kuna mambo mazuri yanakuja baada ya kuwaona vijana na kuhusu kurejea katika nafasi yangu, nitatoa tamko siku chache zijazo,” alisema.

Hata hivyo, uwepo kwa Manji Uwanja wa Taifa, uliwafanya mashabiki waliojazana uwanjani hapo kuwa na furaha, kwani hawakutarajia kama wangemuona licha ya mabosi wa klabu yao kutangaza mapema kuwa, atakuwa mmoja wa wageni katika mchezo huo ambao Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo ndiye aliyekuwa Mgeni Rasmi.

Sasa unaambiwa mara baada ya Manji kutoka chumbani alikwenda moja kwa moja kwenye chumba cha wachezaji na kuzungumza nao akiwaambia anataka washinde ili kumpa heshima Rais Dk. John Magufuli na kweli vijana wakafanya kweli uwanjani.

Wachezaji wa Yanga waliocheza kwa morali walijazwa upepo pia na Jenerali Mabeyo, aliyewaambia akiwa na Manji kuwa, taifa zima lipo nyuma yao katika mchezo huo, hivyo wasiaangushe na kweli jeshi hilo la Mwinyi Zahera likapambana na kushinda mchezo huo.

Licha ya ushindi huo kutoisaidia Yanga kutoka mkiani kutokana na Rayon Sports ya Rwanda kushinda ugenini mabao 2-1 dhidi ya Gor Mahia, lakini umekuwa faraja kubwa kwa mashabiki wa Yanga kwani, timu imecheza mpira mwingi tofauti na mechi zilizotangulia.

KASEKE, MAKAMBO NOMA

Jana uwanja mzima ulijawa mzuka, ambapo kila bao lilipofungwa mashabiki walikuwa wakishangilia kwa kukitaja cheo cha Jenerali Mabeyo...CDF kisha wanamalizia na Manjii. Staili hiyo ilikuwa ikiwapa mzuka wachezaji, ambapo Deus Kaseke aliyekuwa akicheza mechi yake ya pili ya CAF, aliiandikia Yanga bao la kwanza dakika 44 akiiwahi pasi ya nyuma ya mabeki wa USM, bao lililoamsha hoihoi uwanjani kabla ya Mkongoman Heritier Makambo kuongeza la pili dakika chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili. Makambo katika mchezo huo alionyesha uwezo wa hali ya juu akishirikiana na kina Papy Kabamba Tshishimbi na Kaseke kuwasimamisha Waarabu hao, ambao wamepoteza mchezo wa kwanza jana na kuendelea kubanana na Gor Mahia ya Kenya iliyolala nyumbani mbele ya Rayon Sports.

Straika huyo aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na uzi wa Yanga, alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi murua ya Kaseke na kumchambua kipa wa USM, Mohammed Zemmamouche.

Hata hivyo, dakika chache baadaye shuti kali la nje ya boksi la Abderrahim Meziane, lilimshinda nguvu kipa Beno Kakolanya na kuipa USM bao pekee la kufutia machozi. Ushindi wa jana umeifanya Yanga kufikisha pointi nne na kuendeleza rekodi yao ya kuzinyoa timu za Kaskazini kwenye mechi za nyumbani tangu walipovunja mwiko wa miaka 32 dhidi ya Al Ahly ya Misri waliyoilaza bao 1-0 mwaka 2014.