Mapacha waliotenganishwa Muhimbili watoka hospitalini

Muktasari:

Mapacha waliotenganishwa Muhimbili waruhusiwa kwenda nyumbani, mama yao ashukuru hospitali na wauguzi kuwa naye karibu

Dar es Salaam. Baada ya kukaa hospitalini kwa miezi minne, hatimaye watoto pacha; Gracious na Precious Mkono waliotenganishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wameruhusiwa kurudi nyumbani.

Pacha hao walifanyiwa upasuaji wa kihistoria wa kuwatenganisha Septemba 23, 2018 katika hospitali hiyo baada ya kuzaliwa wakiwa wameungana sehemu ya kifua na tumbo.

Akizungumza akiwa na uso wenye tabasamu leo Ijumaa Novemba 9, 2018, mama wa watoto hao, Esther Mkono amesema ni furaha ya aina yake kurejea nyumbani akiwa na watoto wake wakiwa salama.

Mkono ameiambia Mwananchi Digital kuwa amepatiwa huduma nzuri na wauguzi walikuwa wakimuangalia kwa karibu kama ndugu yao.

“Nashukuru leo narudi nyumbani nikiwa na watoto wangu wote wako salama, hospitali imekuwa na msaada mkubwa kwangu hadi kufikia leo,” amesema huku akiingia kwenye gari lililokuwa likimsubiri kwa ajili ya safari ya kwenda nyumbani Kisarawe mkoani Pwani.

Awali, watoto hao walitakiwa kuruhusiwa wiki mbili zilizopita, lakini uongozi wa hospitali ulisitisha uamuzi huo kutokana na sababu za kimazingira.

Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto MNH, Petronila Ngiloi alisema walitarajia kuwaruhusu mapema, lakini tatizo ni maisha halisi ya familia hiyo, ambapo watoto hao wangeshindwa kumudu.