Mapya yaibuka mwamuzi wa Simba SC, KMC

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Salum Chama, amesema haitamtumia tena aliyekuwa mwamuzi wa kati katika mchezo baina ya KMC na Simba, Abdallah Kambuzi wa Shinyanga.

Wakati sakata hilo likiwa halijapoa, imefichuka mwamuzi aliyepangwa kuchezesha mchezo huo alikuwa Martine Saanya wa Morogoro na si Kambuzi.

Kambuzi alichezesha mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao Simba ilishinda mabao 2-1 Uwanja wa CCM Kirumba, Alhamisi iliyopita.

Kambuzi na wasaidizi wake, Godfrey Msakila (Geita) na Consolata Lazaro (Mwanza) waliondolewa katika orodha ya waamuzi katika mechi zote zilizobaki msimu huu.

Taarifa iliyotolewa na TFF muda mfupi baada ya mechi hiyo, ilisema waamuzi hao wameondolewa baada ya kuonyesha kiwango kisichoridhisha katika mchezo huo.

Akizungumza jana, Chama alidai kamati ya waamuzi imeamua kumuondoa Kambuzi katika orodha yake kwa kuwa amekuwa akifanya makosa ya kujirudia mara kwa mara.

“Kanuni za CAF (Shirikisho la Soka Afrika) na Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa) zinasema mwamuzi afungiwe si zaidi ya miezi sita, lakini miaka miwili au mitatu ni kama umemfuta.

“Adhabu ya miezi mitatu au sita maana yake ni mtu ajirekebishe, lakini kwa Kambuzi hii ni adhabu yake ya tatu, anafanya makosa yaleyale, hivyo kamati tumeamua kutomtumia tena,” alisema Chama.

Aidha, Chama alisema mwamuzi aliyepangwa kuchezesha mchezo huo alikuwa Saanya kabla ya kubadilishwa na kuteuliwa Kambuzi baada ya Saanya kukosa ruhusa.

“Martin Saanya ndiye alipangwa kuwa mwamuzi wa kati, lakini siku mbili kabla ya mechi aliomba udhuru kwa sababu ya changamoto ya ruhusa kazini kwake, lakini waamuzi wa pembeni hawakubadilishwa.

“Kambuzi alikuwa mwamuzi wa akiba, mmoja wa wajumbe wetu alimpendekeza awe mwamuzi wa kati na kamati ikaridhia, kama inatokea mwamuzi aliyepangwa ameomba udhuru ‘desk officer’ wetu analeta katika ‘group’ tunapendekeza au yeye anampendekeza mwamuzi mwingine na kamati inamjadili kabla ya kumpitisha,” alifafanua Chama.

Pia Chama alifafanua mchakato uliotumika kutoa adhabu ya Kambuzi na wenzake kuwa ingawa uamuzi unafanywa na Kamati ya saa 72, lakini waamuzi hao wasingeachwa hadi kamati hiyo ikutane kulingana na kosa.

“Kamati ya saa 72 ndiyo inatoa uamuzi baada ya kupitia ripoti ya mwamuzi, kamisaa na msimamizi wa mchezo, lakini kwa akina Kambuzi wasingesubiri kamati kwasababu kabla kamati haijakutana kuna mechi walipangwa kuchezesha wakati mechi iliyopita wamevuruga,” alisema Chama.

Liunda, Kazi wafunguka

Wakizungumzia adhabu ya waamuzi hao, Mkufunzi wa Waamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Mjumbe wa Kamati ya Waamuzi Tanzania, Leslie Liunda alisema adhabu za waamuzi inategemea na mahitaji ya wakati huo.

“Hata Katibu Mkuu wa TFF kupitia ofisi yake anaweza kutoa adhabu kwa waamuzi bila kusubiri Kamati ya Saa 72,” alisema Liunda jana.

Mwamuzi wa zamani, Othman Kazi alisema huenda Kambuzi aliteleza kwa kufanya makosa aliyodai ya kibinadamu, lakini aliponzwa na wasaidizi.

“Kwangu sioni kosa la Kambuzi katika mechi ile hadi kufungiwa, lakini uamuzi wa kufungiwa umetolewa haraka tena siku ya Sikukuu,” alisema.