Maradona: Argentina inakwenda Russia kutalii

Muktasari:

  • Maradona alisema Argentina haiwezi kupata mafanikio katika fainali hizo kwa kuwa haina kiongozi bora na mpango mkakati wa kushinda mechi zake hivyo inakwenda Russia kutalii.

Buenos Aires, Argentina. Gwiji wa zamani Argentina, Diego Maradona amesema hana matumaini na kikosi hicho katika fainali za Kombe la Dunia.

Maradona alisema Argentina haiwezi kupata mafanikio katika fainali hizo kwa kuwa haina kiongozi bora na mpango mkakati wa kushinda mechi zake hivyo inakwenda Russia kutalii.

Nahodha huyo wa zamani aliyeipa Argentina Kombe la Dunia mwaka 1986 nchini Mexico, alisema timu hiyo inaweza kupenya katika hatua ya awali, lakini haitasonga mbele.

“Nina hofu, nina hofu sana kama inaweza kuvuka katika hatua ya awali dhidi ya Nigeria, Iceland na Croatia, lakini haitakuwa kazi rahisi,” alionya Maradona aliyejiuzulu kuinoa timu ya Daraja la Pili Al-Fujairah ya Falme za Kiarabu mwezi uliopita.

Nguli huyo alisema Argentina inaundwa na wachezaji wasiokuwa na uzoefu ambao wamekosa mpango mkakati na hawawezi kucheza kwa mafanikio.

Alisema ana amini timu hiyo inakwenda kucheza kamari Russia kwa sababu imejaza wachezaji wanaotaka kwenda kuonyesha ufahari katika mashindano hayo.

Maradona ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Dynamo Brest ya Belarus, amekosoa mbinu za kocha Jorge Sampaoli kwa kutumia mfumo 2-3-3-2 aliodai ulikuwa ukitumika mwaka 1930.