Martinez ajivua lawama kwa Man United

Muktasari:

  • Kocha wa timu ya Taifa ya Ubelgiji Roberto Martinez, amejivua lawama ni kama ameamua kujivua lawama kutoka kwa kocha wa Manchester United, Jose Mourinho kwa kuamua kutomchezesha Marouane Fellaini ambaye ndiye kwanza amepona majeraha, katika mechi ya kirafiki dhidi ya Uholanzi iliyochezwa jana.

London, England. Kocha wa timu ya Taifa ya Ubelgiji, Roberto Martinez, amejivua lawama kwa benchi la ufundi la Manchester United, baada ya kuamua kutomtumia kiungo Marouane Fellaini, katika mechi ya kirafiki dhidi ya Uholanzi juzi.

Kocha huyo mara kadhaa alilalamikiwa na kocha wa Man United, Jose Mourinho, kwamba amekuwa akimtumia Fellaini bila kujali suala la majeruhi jambo linalomuongezea hatari ya kukosa mechi nyingi.

Martinez hakumtumia Fellaini katika mchezo wa kirafiki uliopigwa juzi dhidi ya Uholanzi uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 ili kukwepa lawa kutoka kwa Man United inayotaka kumtumia kwa mchezo wa Jumamosi hii dhidi ya Chelsea.

Kiungo huyo alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya nyonga jambo lililokuwa likimpa hofu kocha wa Man United, Jose Mourinho ambaye anatamani kushinda mechi dhidi ya Chelsea ili kukinusuru kibarua chake.

“Napenda kuweka wazi kuwa Fellaini kwa sasa yupo vizuri, nadhani Man United, inaweza kumtumia katika mechi yake ya Jumamosi dhidi ya Chelsea maendeleo yake ni mazuri, hakucheza mchezo wa Ubelgiji dhidi ya Uholanzi kwa sababu ya kumpa nafasi ya kupona kwa asilimia 100,” alisema Martinez.

Mourinho anautolea macho mchezo huo wa Jumamosi kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, kutokana na umuhimu wa ushindi katika kukinusu kibarua chake ambacho hakipo salama sana kutokana na matokeo ya msimu huu.

Man United imepoteza mechi tatu hadi sasa katika michezo minane iliyocheza imejikusanyia pointi 13, ikiwa pointi saba nyuma ya vinara wa ligi hiyo Man City, Liverpool na Chelsea ambazo hazijapoteza mchezo hata mmoja hadi sasa.