Mnadani yainyuka Mwanza Terminal Ndondo Cup

Muktasari:

  • Mashindano hayo yameingia katika hatua ya nusu fainali

Mwanza. Mnadani FC imefuzu kwa nusu fainali ya mashindano ya Ndondo Cup kwa kuichapa Mwanza Terminal kwa bao 1-0, huku burudani ya kipekee ikiwa kwa mashabiki nje ya uwanja kwa jinsi wanavyopambana kusaka kitita cha Sh 1 milioni.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Nyamagana, mashabiki wa Power FC pamoja na timu yao kuwa imeshatolewa nje, walikuwa kivutio kwa jinsi walivyotinga uwanjani na mfano wa mtumbwi na kasia.

Mashabiki hao walifika uwanjani dakika ya 17 ya mchezo, ghafla waliwazima wapinzani wao Mnadani ambao wao waliingia na Baro la Mtumba na mtu aliyevalia mithiri ya mwanamwari wakishangilia.

Ilikuwa ni burudani ya aina yake kwa jinsi mashabiki hao walivyokuwa wakizunguka uwanja mzima wakiwa wamembeba mfalme wao juu kwa juu akipiga kasia na kuwaamshia shangwe wadau waliojitokeza.

Akizungumza na gazeti hili kiongozi wa kundi hilo la Power, Khatib Mussa alisema kuwa wamejipanga kimkakati kuhakikisha wanachomoza na kitita cha Sh 1 milioni.

“Hatuoni kundi lolote lenye kutuzuia kuchukua ubingwa wa kundi bora la ushangiliaji, tumejipanga na kila siku tutakuwa tunakuja na kitu tofauti,” alisema Mussa.

Naye mmoja wa mashabiki wa Mnadani, Juma Owio alisema kuwa licha ya mbwembwe za wapinzani wa Power wanazotamba nazo, haziwapi presha kwani wao wapo juu.

“Hiyo ni mikwara tu wala hatuogopi, sisi ni kundi kubwa na watatukoma mechi ijayo wajipange kwetu watachemka” alitamba Shabiki huyo aliyekuwa amevalia vazi ‘Bi Harusi’ akipigiwa vigeregere.