Majeruhi wazidi kuwaandama Simba

Tuesday October 17 2017

 

By Thobias Sebastian, Charles Abel

Dar es Salaam. Simba itamkosa beki wake Salim Mbonde katika mchezo minne ijayo ukiwamo ule wa watani wa jadi dhidi ya Yanga.

Simba inaendelea kujifua kwenye Uwanja wa  wa Polisi College Kurasini kujiandaa na mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Njombe Mji itakayochezwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Uhuru..

Akizungumza na wanahabari leo Ofisa habari wa Simba, Haji Manara alisema Simba ina majeruhi ya wachezaji wanne  Shomari Kapombe, John Bocco, Said Mohamed ‘Nduda’ na Salim Mbonde ambao wameshindwa kufanya mazoezi na wenzao.

Manara alisema baada ya mechi  dhidi ya Mtibwa Sugar iliyomalizika kwa sare bao 1-1, idadi ya majeruhi imeongeza katika kikosi chao.

"Beki wetu Mbonde katika mechi ya Mtibwa alipata maumivu ya goti ambayo yatasababisha kukosa mechi nne ambazo kati yake itakuwa dhidi ya Yanga"

Manara alisema mshambuliaji John Bocco alipata majeruhi ya kisigino katika mechi hiyo na Mtibwa, atakuwa nje kwa wiki moja na atakosa mechi dhidi ya Njombe Mji ila atakuwepo katika mechi ijayo dhidi ya Yanga.

"Kapombe ni mchezaji tunaamini atatusaidia kwani bila shaka hakuna mpenzi wa Simba asiyefahamu uwezo wa mchezaji huyo ambaye alianza kuonekana akiwa hapa, kwahiyo tunaomba mashabiki wetu, wavumilie juu ya hilo," alisema Manara.

"Kipa Nduda atakuwa nje kwa wiki nane ili kupona kabisa na kuanza mazoezi na kuangalia kama anaweza kujiunga na timu au kuendelea na matibabu zaidi ya hapo."

Manara alisema mechi yao dhidi ya Njombe itakuwa ya kulipiza machungu ya sare waliyoyapata katika mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa sugar.

Katika hatua nyingine viongozi wa Simba wameupongeza  uongozi mpya wa bodi ya ligi iliyochaguliwa Jumapili ya wiki iliyopita.

"Tunaimani Bodi hii itakuwa ya huru na haki kwani tunafahamu Mwenyekiti wake aliyechaguliwa Clement Sanga atakuwa anafanya uamuzi ya huru na haki," alisema.
"Tunafahamu kuwa Sanga ni kiongozi wa juu wa Yanga ila kwa uadilifu na ufanisi wake wa kazi tunaimani itakwenda kufanya kazi ya bodi ya ligi bila ya kubezi upande wa Yanga au Simba na kila timu itapata kile ambacho itakuwa inastahili kutoka kwa bodi hiyo," alisema Manara.

 

Advertisement