Mastaa wanne waiweka mtegoni Mbao FC

Kocha wa Mbao FC Amri Said

Muktasari:

  • Klabu ya Mbao imepata pigo baada ya kuripotiwa taarifa huenda ikawakosa wachezaji wanne waandamizi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.
  • Kocha wa Mbao Amri Said aliwataja wachezaji hao ni  Yusuph Mgeta, David Mwassa, Lorand Msoje na Helbert Lukindo ambao ni majeruhi.

Mwanza. Kocha wa Mbao FC Amri Said anatarajiwa kuwakosa wachezaji wanne waandamizi katika mchezo wa Jumapili dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Akizungumza mjini hapa jana, Said alisema hana uhakika wa kuwatumia wachezaji Yusuph Mgeta, David Mwassa, Lorand Msoje na Helbert Lukindo ambao ni majeruhi.

Kocha huyo wa zamani wa Lipuli, alisema Mwasa ambaye ni nahodha wa timu hiyo ameanza mazoezi mepesi, lakini hana uhakika kama atacheza.

Said, beki wa zamani wa Simba, alisema Mgera ana majeruhi ya kifundo cha mguu, Lukindo na Msonje wamepata maumivu ya goti.

Kocha alisema ana wachezaji wengine watakaoziba nafasi zao na tayari amewapa majukumu katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa na msisimko.

“Mechi mbili tulizopoteza tulifanya makosa katika safu ya ushambuliaji ambayo ilishindwa kufunga mabao, wakati tukisubiri mechi ya Jumapili naendelea kuwapa mafunzo na mbinu za ushindi,”alisema Said.

Mara ya mwisho Mbao na Mtibwa Sugar zilitoka suluhu  msimu uliopita  katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja huo timu hiyo ilikuwa chini ya Kocha Ettiene Ndayiragije aliyetimkia KMC.