Matheo anukia Kagera Sugar

Muktasari:

Matheo alikuwa akiwaniwa na klabu nyingi za ligi kuu na Kagera ndiyo wenye nafasi ya kumtwaa.

KAGERA Sugar ipo katika hatua za mwisho kumpata straika,  Matheo Antony  kutoka klabu ya Yanga kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Kocha Mkuu wa Kagera, Mecky Maxime amesema, wamekuwa katika mazungumzo ya muda mrefu na Yanga ili kumpata Matheo ambaye amekuwa akiwaniwa na klabu nyingi.

Maxime amesema, alikutana na kocha wa Yanga,  George Lwandamina wakati timu hizo mbili zilipokutana, akamuomba mshambuliaji huyo kwa mkopo ombi ambalo lilikubaliwa na akapewa masharti ambayo Maxime hakutaka kuyaweka wazi.

Amesema, baada ya kukubaliwa ombi hilo na Lwandamina,  waliwasiliana na uongozi wa Yanga na sasa wameshafunguliwa milango ya kuongea na mshambuliaji huyo ili aweze kutua kwao kwa mkopo.

"Namjua Matheo ni mshambuliaji mdogo na mwenye kipaji sidhani kama Yanga hafai lakini amekuwa akikosa nafasi nimewaomba Yanga wanipe kwa mkopo ili aje huku kuboresha uwezo wake na nashukuru tumekubaliwa,"amesema Maxime.