Simba washindwe wenyewe tu Afrika

Muktasari:

Mabingwa hao wa Kombe la FA wanashiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo tangu 2012

SIMBA na Yanga zimeanza kupiga hesabu juu ya ushiriki wao wa michuano ya kimataifa, lakini Wekundu wa Msimbazi wametabiriwa kufika mbali zaidi kuliko Yanga na sababu zake zikatolewa kiroho safi.

Imeelezwa mfumo wa uchezaji wa Simba kutomtegemea mchezaji mmoja kufunga ndio itakayowapiga bao watani zao Yanga katika michuano hiyo.

Simba imepangwa na Gendarmerie National ya Djibout, wakati ya Yanga itaanza na St Louis ya Shelisheli katika mechi za raundi ya awali zitakazochezwa kati ya Feb 9-18.

Mchambuzi mahiri wa soka nchini, Ally Mayay alisema kuwa, mfumo wa Simba wanavyotumia viungo wengi wenye uwezo wa kupanda kwa pamoja eneo la kufunga na matokeo yake, Ibrahim Mohammed 'MO', Mzamiru Yasin, Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi na Said Ndemla wakafunga.

Akitofautisha na Yanga aliodai wanashambulia zaidi kutokea pembeni na kumweka straika mmoja mbele kumalizia, kitu alichodai endapo kama Amissi Tambwe na Donald Ngoma, hawatakuwa fiti Yanga itapata wakati mgumu.

Mayay aliyewahi kuichezea Yanga na Taifa Stars alisema kwa sasa Yanga hakuna aliyemudu kucheza kama Simon Msuva, aliyekuwa akiibeba timu hiyo akianzisha mashambulizi na kufunga, hivyo Yanga ijipange kwelikweli.

"Sina hakika wametumiaje dirisha dogo la usajili, lakini njia mbadala klabu zote mbili, zijipange kushinda nyumbani ugenini iwe sare kama wanavyofanya Waarabu, hilo litawafanikisha," alisema

Mabeki wa zamani wa Simba, Amri Said na Frank Kasanga 'Bwalya' kila mmoja aliitaja Simba kama itakayonufaika na mfumo wa uchezaji wao katika mechi hizo, japo wamezitaka zote zijipange kama zinataka zifike mbali.

Bwalya alitoa tathimini yake kwa timu zote mbili na kusema kama hazikusajili vema kupitia dirisha dogo, basi mabechi ya ufundi yatumia plani B kuweza kujiweka vema.

"Simba inaonekana kubebwa na viungo wanajiongeza na ndio maana unakuta mastraika hawatazamwi kwa jicho la ndani, Yanga wanatumia mastraika halisia, sasa waombe Ngoma na Tambwe, warejee kwenye nafasi yao haraka,"

"Chirwa ni mzuri, lakini anapocheza na Ajibu bado kombinesheni yao haijakaa vizuri, nje ya wachezaji wanaokaa mbele, upande wa mabeki Yanga wapo imara," alisema nyota huo wa zamani wa Msimbazi.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Muhidin Ndolanga  aliwahi kukariwa akisema Simba na Yanga, zinapaswa kujitathimini kujua kwa nini miaka yote wanakwama katika michuano hiyo.

"Uhalisia wa mastaa wao, kipimo chake ni kwenye michuano ya kimataifa, hapo utajua sifa wanazopewa zinaendana na kazi yao, la sivyo lazima wajue kusajili na kuandaa timu za vijana kuanzia ngazi ya chini kabisa," alisema.