Mazoezi Yanga usipime kabisa

Muktasari:

  • Zahera alisema kuwa anashughulikia zaidi mambo matatu anayohaona yanahitajika zaidi kwa sasa ambayo ni pumzi, stamina na ufundi.

Morogoro. Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ameendelea kuiongezea makali timu yake inayojiandaa kumalizia mechi za mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018/19.

Zahera alisema kuwa anashughulikia zaidi mambo matatu anayohaona yanahitajika zaidi kwa sasa ambayo ni pumzi, stamina na ufundi.

Pumzi ya kutosha

Akimaliza siku ya 11 jana akiwa na kikosi chake kambini mkoani Morogoro, Zahera ameonekana kutilia mkazo mkubwa pumzi ya wachezaji wake katika maandalizi hayo.

Wakiwa hapa Zahera amekuwa kila baada ya siku mbili anarudisha dozi ya mazoezi ya pumzi ambapo mazoezi hayo yamekuwa yakifanyika kwa mbio zenye njia tofauti.

Kocha huyo raia wa DR Congo amekuwa akiwakimbiza wachezaji wake kwa mbio za kasi kubwa akitaka kuona ndani ya sekunde tano vijana wake wanafika katika kituo kimoja huku wakati mwingine akiwataka kukimbia huku wakichezea mpira.

Zoezi hilo linaonekana kuwapa uhai wachezaji wake ambapo katika mchezo wa juzi dhidi ya timu ya Morogoro Tanzanite Academy licha ya ushindi walioupata wa mabao 5-1 Yanga ilionekana kuwa imara kwa pumzi ikiwasadia kutengeneza mashambulizi na kukaba kwa haraka

Stamina

Wachezaji wa Yanga sasa wanaonekana kuwa imara kwa nguvu ya mwili ambapo sio rahisi kuweza kuwapokonya mipira wanapombana kwa mwili.

Kocha huyo amekuwa akiwafanyisha vijana wake mazoezi ya kuongeza nguvu ambapo jana aliwataka wachezaji wake kugawana wawili wawili huku mmoja akimshika miguu mwenzake kwa nyuma na aliyeshikwa kutembea kwa mikono kwa dakika moja na nusu.

Zoezi hilo liliwapa wakati mgumu wachezaji wengi ambapo kocha huyo alifahamu na kuwaambia kuwa kila mmoja afanye kwa kiwango anachokitaka.

Ufundi

Katika mazoezi ya jioni Zahera amekuwa akiwabadilishia dozi wachezaji wake akihamia katika mazoezi ya ufundi wa uwanjani ambapo huko amekuwa akiwapa mbinu mbalimbali za uwanjani ili kupata matokeo mazuri.