Mbao kupoza machungu kwa Simba

Muktasari:

Tangu ipande Ligi Kuu msimu uliopita Mbao haijawai kuifunga Simba zaidi ya kupata sare moja tu.



Mwanza. Baada ya kuondolewa katika mashindano ya Kombe la FA (ASFC), Mbao FC imesema sasa nguvu zao zote wanazihamishia kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Simba kuhakikisha wanashinda.

Timu hiyo  msimu uliopita walifanikiwa kufika fainali ya mashindano ya Kombe la ASFC, lakini msimu huu wameondolewa mapema na Njombe Mji kwa penalti 6-5 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Nahodha wa timu hiyo, Yusuph Ndikumana alisema licha ya kushindwa kusonga mbele, sasa wanageukia mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Simba utakaopigwa Februari 26 Jijini Dar es Salaam.

Alisema wanaamini mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na ushindani wa wapinzani wao walionao, lakini watapambana kuhakikisha wanashinda.

“Haya matokeo yametusikitisha sana, lakini ndio mambo ya mpira lazima tukubali, hapa nguvu zetu tunazielekeza kwenye mechi yetu na Simba kuhakikisha tunashinda”alisema Ndikumana.

Beki huyo Mrundi alisema licha ya Ligi kuwa ngumu, lakini hawatakata tamaa na badala yake wataendelea kusaka ushindi kwenye mechi zilizobaki iwe nyumbani au ugenini.

“Bado tunahitaji ushindi zaidi ili kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu, pointi zetu bado hazitoshi kujihakikishia usalama, tunaenda kwa Simba kusaka ushindi tu,” alisisitiza nyota huyo.

Mbao iliyopo nafasi ya tisa ikiwa pointi 19 itawavaa Simba wanaoongoza Ligi kwa alama 42 ikiwa haijawahi kuwafunga katika mechi nne walizokutana ikiwamo ya fainali ya Kombe la FA mwaka jana.

Simba ilianza kuichapa Mbao FC bao 1-0 Jijini Dar es Salaam, kisha kuwalaza mabao 3-2 uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, ikaichapa tena mabao 2-1 mechi yao ya fainali ya mashindano ya FA mkoani Dodoma na msimu huu zilitoka sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.