Mbao yasaka makali yake

Tuesday November 21 2017

 

By Saddam Sadick,Mwananchi [email protected]

Mwanza. Baada ya kucheza dakika 810 (sawa na mechi tisa), bila ya kupata ushindi kocha msaidizi wa Mbao FC, Ahmad Ally amesema bado bahati yao haijafika

Mbao yenye maskani yake Sabasaba wilayani Ilemela jijini Mwanza, ilimeshinda mechi moja ya ufunguzi wa ligi dhidi ya Kagera Sugar, Agosti 26 mwaka huu mjini Bukoba.

Tangu hapo imekuwa ya kuchezea sare na vichapo na sasa ipo nafasi ya 13 kwa pointi nane baada ya kushuka uwanjani mara kumi.

Kocha Ally alisema kuwa kiufundi vijana wanacheza vizuri, lakini tatizo ni bahati ya kupata ushindi ndio hawajapata na kwamba anaamini watafanya vizuri.

Alikiri ligi ya msimu huu ni ngumu kutokana na kila timu kujipanga kimkakati kusaka pointi tatu ili kujiweka nafasi nzuri.

“Ni kweli tumepata ushindi mmoja kwenye mechi kumi, si kwamba ni matakwa yetu, hata sisi tunahitaji kushinda, lakini ligi ni ngumu, timu zinajiandaa kwelikweli,” alisema Ally.

Aliongeza kuwa wao wanawaandaa vyema vijana kabla ya mechi na wanaridhika wamekomaa, lakini matokeo ya dakika 90 yanawashangaza.

Alisisitiza kuwa hawatakata tamaa hadi kumalizika kwa ligi na kwamba wadau wa soka na wapenzi wa timu hiyo watarajie mazuri hapo mbeleni.

“Haya matokeo hata sisi yanatuumiza,lakini ndio mpira hata Yanga wametoka sare mechi tano, kwahiyo ligi ni ngumu ila tutarudi na watatukubali, kumbuka mechi nyingi tumecheza ugenini,” alisema Kocha huyo.

Kati ya mechi kumi, Mbao imecheza mechi sita ugenini, nyumbani ikicheza minne imevuna pointi nne tu.

 

 

Advertisement