Mbao yapiga hodi Yanga

Muktasari:

Mbao inayomilikiwa na wafanya biashara wa Mbao Mwanza, ipo katika nafasi ya 13, kwenye msimamo wa ligi kuu, wenye timu 16, zinazoongozwa na Simba yenye pointi 22.

KLABU ya Mbao FC ya jijini Mwanza, imeweka mikakati ya kusajili wachezaji kutoka Yanga, lakini wale ambao walikosa nafasi ya kucheza katika mechi  za Ligi Kuu Bara.

Wachezaji wanaowataka ni pamoja na kiungo, Maker Edward ambaye hajacheza mchezo hata mmoja wa ligi kuu, pamoja na Yusuph Mhilu ambaye pia, hakupata  nafasi ya kudumu kikosi cha kwanza.

Mbao imefikia maamuzi ya kufanya mchakato huo,  kutokana kikosi chao kutokuwa na matokeo mazuri. Hadi sasa timu hiyo inayomilikiwa na wafanya biashara wa Mbao wa Mwanza, ipo katika nafasi ya 13, kwenye msimamo wa ligi kuu wenye timu 16, zinazoongozwa na Simba yenye pointi 22.

Nafasi hiyo, ni dalili mbaya kwa Mbao kwani wasipokuwa makini, wanaweza kukumbwa na balaa la kushuka daraja.