Mbaya wa kipa Yanga SC afunguka kupokwa mpira

Mwamuzi wa mechi ya Yanga na Stand United,Benedict Magai (kulia) akimkabizi mpira mshambuliaji wa Stand United,Alex Kitenge baada ya kufunga magoli 3 katika mechi iyo ya Ligi Kuu Bara. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Kitenge raia wa Burundi, alifunga mabao hayo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao Yanga ilishinda 4-3 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limempoka mpira mshambuliaji wa Stand United, Alex Kitenge baada ya kufunga mabao matatu ‘hat trick’ dhidi ya Yanga.

Kitenge raia wa Burundi, alifunga mabao hayo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao Yanga ilishinda 4-3 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Miongoni mwa Kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), inasema mchezaji aliyefunga mabao matatu katika mchezo mmoja anatakiwa kupewa mpira uliotumika katika mechi husika.

Akizungumza kwa simu jana, Kitenge alisema amesikitishwa na uamuzi wa kupokwa mpira na maofisa aliodai wa TFF muda mfupi baada ya mchezo kumalizika.

Kitenge alisema alipiga picha na vigogo wa TFF kabla ya kutakiwa kurudishwa kwa wahusika kwa ahadi kuwa angepewa mpira mwingine.

“Najisikia vibaya kwa sababu mpira huo ni haki yangu na sijui ni lini kocha atakwenda kufuata, nahitaji uwekwe kwenye rekodi ya kazi yangu ninayoendelea kufanya katika soka,” alisema Kitenge.

Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo alisema Kitenge aliambiwa kwenda kuchukua mpira wake makao makuu ya shirikisho hilo, Karume jijini Dar es Salaam.

“Baada ya mechi tulimkabidhi mpira kama mfano kwa sababu mpira ule si ile inayotumika kwenye Ligi Kuu.

Mpira ule ni wa CAF ambayo inatumika kwenye mashindano ya kimataifa na ndiyo inayotumiwa na timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, siku ile ya mchezo ililetwa uwanjani kwa makosa,” alisema Ndimbo.