Mbelgiji: Simba hatupaki basi kwa Nkana

Muktasari:

  • Simba na Nkana zinakutana kwa mara ya kwanza baada miaka 15 kupita mara ya mwisho zilipokutana katika hatua hii Simba ilitolewa kwa jumla ya mabao 4-3.

Dar es Salaam. Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba wameondoka leo kwenda Zambia, huku wakiweka wazi hatacheza kwa kujilinda dhidi ya Nkana katika mchezo wa kwanza kusaka kufuzu kwa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa utakaopigwa jijini Kitwe Jumamosi hii.

Simba ilichakaza Mbabane Swallows kwa Eswatini kwa jumla ya mabao 8-1 katika raundi ya awali na kupata nafasi ya kucheza na Nkana ambayo ilitoa UD Songo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 3-1.

Kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems ameweka wazi kuwa lengo lake la kwanza ni kushinda mechi hiyo, huku akikiri kuwa haitakuwa rahisi kwa sababu wanakutana na timu bora ugenini.

Aussems kocha wa zamani wa AC Leopards, Nepal amesema hataki kuingia katika mchezo huo kwa lengo la kupata sare ya ugenini ili aweze kuiondoa Nkana akiwa nyumbani, badala yake atacheza soka la kushambulia  kama ilivyokuwa dhidi ya Mbabane na kupata ushindi mnono ugenini.

“Sina wachezaji wanaojilinda. Nina wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kushambulia, kwa hiyo tunakwenda kusaka ushindi ugenini,” alisema baada ya kumaliza mazoezi ya mwisho Dar es Salaam kabla ya kuondoka kwenda Kitwe alfajili ya leo Jumatano.

“Tumefanya mazoezi kwa siku chache Dar es Salaam, ni matumaini yangu mazoezi yetu ya mwisho Kitwe yatatuweka katika hali nzuri zaidi kwa mchezo huo,” aliongeza Mbelgiji huyo.

Hata hivyo, Aussems alitoa heshima kwa Nkana akisema ni timu tofauti na wapinzani bora, hivyo mechi hiyo itakuwa ngumu tofauti na ile ya Mbabane.

“Yote tuliyofanya dhidi ya Mbabane sasa yamebaki historia. Nkana ni timu mzuri, tunatakiwa kucheza vizuri zaidi. Lengo letu ni kuhakikisha tunafunga mabao zaidi yao, hicho ndicho tunachokwenda kufanya katika mchezo huu,” alisema Aussems.

Nahodha wa Simba, John Bocco alisema mchezo huo utakuwa mgumu kuliko uliopita, lakini kama tutajianda vizuri na kufuata maelekezo ya kocha na kucheza vizuri tutashinda.

“Maandalizi yetu ya mchezo huu yamekwenda vizuri kama yalivyopangwa. Matumaini yetu tutakuwa na mchezo mzuri ikiwezekana tutashinda ugenini,” alisema mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara 2017/18.

“Ushindi tuliopata katika mchezo uliopita umetuongezea nguvu, japokuwa sasa mambo yatakuwa tofauti kidogo. Tunaanza mechi yetu ya kwanza ugenini, hivyo tunatakiwa kuwa makini zaidi. Naamini kocha atakuja na mbinu bora ya mchezo huu,” aliongeza mshambuliaji huyo.