Mbelgiji Simba sasa ni zamu ya Yanga

Muktasari:

  • Simba na Yanga zinakutana katika Ligi Kuu Bara kwa mara 101 tangu mwaka 1965 ilipoanzishwa ligi hiyo

Shinyanga. Baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mwadui kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema kazi iliyopo mbele yake ni kuhakikisha anaifunga Yanga.

Pamoja na tambo za kutaka kuifunga Yanga, lakini Mbelgiji huyo amesema kupeka kadi nyekundu kwa nahodha wake John Bocco ni pigo kubwa kwao kuelekea mechi hiyo.

Aussems alisema hawakufanya vizuri mechi zilizopita hivyo aliwataka wachezaji wake kucheza kwa tahadhari kubwa kuhakikisha wanashinda kwani hata wapinzani wao walikuwa wazuri.

"Tunashukuru tumeshinda, mechi haikuwa rahisi, nimepata pigo la Bocco kupewa kadi nyekundu lakini nitaangalia cha kufanya kuelekea mechi ijayo ingawa alitakiwa apewe kadi ya njano, nitaangalia picha kuona kama kweli alistahili hiyo kadi.

"Pigo hilo na matokeo haya yananipa picha ya mechi ijayo, kujipanga ni vipi tutakabiliana na wapinzani wetu, Yanga sio timu ya kuibeza na ina ushindani mkubwa, mashabiki wanahitaji ushindi, lakini yote hayo ni mipango.

"Yanga wanafanya vizuri hivyo sidhani kama wanahitaji kupoteza mechi kirahisi ila hata sisi pamoja na matokeo ya nyuma tunahitaji kushinda mechi hiyo," alisema Aussems

Aussems alisema vijana wake hawakucheza vizuri kama mechi yao iliyopita dhidi ya Mbao ingawa hawakupata ushindi kwani hata uwanja umechangia.