Mbelgiji wa Simba azua mapya

Muktasari:

Wakizungumza na mwanaspoti online, mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay amesema kitendo cha timu hiyo kusajili nje ya matakwa ya mwalimu kinaonyesha namna ambavyo hawaheshimu taaluma za watu.

Dar es Salaam. Baada ya uongozi wa Simba kumtangaza rasmi kocha mkuu Mbeligiji Patrick Asseums wadau wa soka wamesema uongozi wa klabu hiyo umerudia makosa yale yale ya kumfanyia usajili.

Wakizungumza na mwanaspoti online, mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay amesema kitendo cha timu hiyo kusajili nje ya matakwa ya mwalimu kinaonyesha namna ambavyo hawaheshimu taaluma za watu.

Alifafanua kauli yake kwamba imekuwa ni kawaida kwa viongozi wa klabu kusajili wachezaji kwa matakwa yao,  lakini mwisho wa siku inakuwa ni kinga kwa kocha kujitetea kama kikosi hakikuwa sahihi kwake.

"Inakuwa ni ngumu kumlaumu kocha kwa nini hajafika kwenye malengo, kwani jibu lake ni rahisi atasema wachezaji haikuwa chaguo lake, sasa inakuaje viongozi wanashindwa kuliona hilo kila msimu wanafanya vitu kwa kujirudia.

"Simba kwa sasa wapo vizuri kiuchumi, lakini tayari wameishasajili wachezaji wengi na kocha anataja sifa za mchezaji anayemtaka sasa je hawaoni kama wanapoteza pesa bila sababu za msingi,' alisema Mayay.

Alisema viongozi hao wanaweza kusingizia kwamba kocha msaidizi Masoud Djuma alikuwepo wakati wa usajili huo, jambo aliloliita sio dawa kwa madai huyo wa sasa naye ana jicho lake la kuona.

"Kinachotakiwa kufanyika ni  Masoud kufanya ushawishi mkubwa kwa Asseums kumuelekeza wachezaji kwa maana ya namna wanavyocheza na tabia zao nje ya uwanja ili ajue pakuanzia na kuwajenga kisaikolojia," alisema Mayay.

Naye kocha Joseph Kanakamfumo alisema ni kawaida kwa viongozi kusajili badala ya kocha hivyo ujio wa mwalimu  Mbelgiji ndani ya kikosi cha Simba itampaswa alazimike kuendana na mifumo yao.

"Akisema aendelee kukomaa na kuhitaji wachezaji chaguo lake atafeli, awatengeze waliopo akisaidiana na msaidizi wake Masoud Djuma ambaye alikuwa anashuhudia wakisajiliwa," alisema kocha huyo.