Mbeya City yamnasa kocha Mrundi

Muktasari:

  • Kocha huyo amepewa mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo ya Mbeya City ambayo ilikuwa ikisimamiwa na kocha msaidizi, Mohammed Kijuso tangu ilipoachana na Mmaalawi Kinnah Phiri.

Dar es Salaam. Wagonga nyundo wa Mbeya City wameipiga bao la kisigino Ndanda FC baada ya kumnasa kocha Ramadhan Nsanzurwimo aliyekuwa mbioni kujiunga na timu hiyo ya Mtwara.

Kocha huyo amepewa mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo ya Mbeya City ambayo ilikuwa ikisimamiwa na kocha msaidizi, Mohammed Kijuso tangu ilipoachana na Mmaalawi Kinnah Phiri.

Kabla ya kujiunga na Mbeya City, Nsazurwimo alikuwa katika hatua za mwisho kuingia mkataba na Ndanda FC, lakini mgogoro wa kiuongozi ulioibuka, ulisababisha mpango huo kuvunjika.

Taarifa iliyotolewa na afisa habari wa Mbeya City, Shah Mjanja imesema kocha huyo ataungana na timu katika kanda ya ziwa ambako ipo kwa sasa ikijiandaa na mechi zake za Ligi Kuu.

Kocha Ramadhani amewahi kuwa kocha kwa nyakati tofauti katika vilabu mbalimbali nchini Burundi, Rwanda, Botswana, Malawi, Uganda, na Afrika ya Kusini, pia amewahi kuwa mshauri wa ufundi katika timu ya taifa ya Burundi na kocha msaidizi na kocha mkuu wa Muda kwa timu ya taifa ya Malawi.