Mbinu aliyotumia Mtanzania kuzamia Madola Australia

Mchezaji tenisi ya meza, Fathiya Pazi

Muktasari:

Akizungumzia tukio hilo kwa simu kutoka Australia jana, mkuu wa msafara Yusuph Singo alisema, mchezaji huyo alipata upenyo wa kutoroka baada ya kuwategea wanamichezo wenzake waliokwenda kunywa chai.

Dar es Salaam. Wakati timu ya Tanzania ikianza safari ya kurejea nchini leo kutoka Australia ilipokwenda kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola, mchezaji tenisi ya meza, Fathiya Pazi ameingia mitini.

Akizungumzia tukio hilo kwa simu kutoka Australia jana, mkuu wa msafara Yusuph Singo alisema, mchezaji huyo alipata upenyo wa kutoroka baada ya kuwategea wanamichezo wenzake waliokwenda kunywa chai.

Singo ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, alidai mchezaji huyo alitimka kambini Ijumaa iliyopita.

“Alisubiri muda ambao wenzake wamekwenda kunywa chai akatumia kuondoka, mwenzake anayekaa naye hosteli (Neema Mwaisyula) aliporejea chumbani hakumkuta.

“Alidhani labda ametoka mara moja na atarejea, lakini hadi usiku hakumwona ndipo akaja kutueleza Fathiya hayupo tangu asubuhi. Matroni alikwenda na Neema kuangalia vitu vyake, akakuta ameacha begi kubwa na suti za michezo, aliondoka na kibegi kingine kidogo,” alisema Singo.

Mkurugenzi huyo alisema walikwenda kuripoti tukio hilo polisi katika Mji wa Gold Coast, lakini waliambiwa hawana uwezo wa kumkamata na kwa mujibu wa sheria za Australia mchezaji huyo hajafanya kosa.

“Polisi walituambia wanachofanya ni kusaidia kujua alipo, lakini hawawezi kumkamata kwa sababu hana kosa kwa kuwa viza yake itakwisha Mei, kama itafika Mei hajarudi ndipo watamtafuta,” alisema Singo.

Alisema uchanguzi wa awali wamebaini mchezaji huyo alinunua ‘laini’ nyingine ya simu ya Australia muda mfupi kabla ya kutokomea kusikojulikana.

“Tumefanikiwa kupata duka alilonunua hiyo ‘laini’, Polisi wameanzia hapo kufuatilia ni wapi alielekea na nani aliwasiliana naye.

“Tunachodhani tukio la kutoroka lilipangwa mapema huenda tangu akiwa nyumbani (Tanzania) na hata ‘laini’ ya simu ya Australia aliyonunua tunahisi aliitumia kuwasiliana na ndugu zake huko nyumbani ili kuwatoa hofu ya mahali alipo.

Singo alisema wamempa taarifa za tukio hilo Katibu Mkuu wa Chama cha Tenisi ya Meza (TTA), Issa Mtalaso kufuatilia suala hilo nyumbani kwao.

Alisema Fathiya ametoroka katika mazingira magumu kwa kuwa pasipoti za wachezaji wote wa Tanzania zipo mikononi mwake.

Mtalaso alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema hawezi kuzungumza hadi timu hiyo itakaporejea nchini ingawa alikiri kwenda nyumbani kwa mchezaji huyo.

Naye Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema bila shaka mchezaji huyo alijiandaa muda mrefu kutoroka.