Mbio za baiskeli kutangaza utalii Rungwe

Muktasari:

  • Mashindano hayo yatakimbia umbali wa kilomita 218 kuzunguka wilaya hiyo

 Zaidi ya waendesha baiskeli 34 kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kesho watafanya utalii wa ndani kwa kupanda mlima Rungwe uliopo katika halmashauri ya Rungwe mkoani Mbeya.

Katibu wa Chama cha Baiskeli mkoani hapa (Mbeca), Patrick Kahise alisema safari hiyo ni mwendelezo wa kauli mbiu yao ya ‘Baiskeli utalii fahari yetu Tanzania’ walioyoianza mapema mwaka huu.

 Kahise alisema waendesha basikeli hao wanatarajia kutoka jijini hapa  kesho saa 2:00 asubuhi kuelekea wilayani hapo ambapo umbali wa safari ni kilomita 218 kwenda na kurudi wakitumia usafiri wa baiskeli.

 Alisema vivutio wanavyotarajia kutembelea daraja la Mungu, maporomoko ya maji, kijungu na vingine vilivyomo ndani ya hifadhi hiyo ya Rungwe inayosifika kwa kuwa na vivutio vya kipekee.

‘’Lengo la kufanya ziara hizo ni kutaka kuwahamasisha watanzania kuwa na utamaduni wa kufanya utalii wa ndani ili tujionee vitu vyetu tulivyonavyo siyo kusubiri tu wageni kutoka mataifa mengine ndiyo watusimulie,’’alisema Kahise.

 Alisema pamoja na kutembelea vivutio hivyo watafika hadi Ziwa Kisimba lililopo umbali wa kilomita 18 kutoka Rungwe mjini.

Mmoja wa waendesha baiskeli kutoka mkoani hapa, Tuntu Sanga alisema lengo waliloanzisha wachezaji hao litatimia kwani wamejipanga kutembelea hifadhi pamoja na mbuga zote zilizopo hapa nchini ili kujenga historia.