Messi aifungia Barca bao la 6,000

Barcelona, Hispania. Nahodha wa Barcelona, Lionel Messi, jana aliifungia timu yake bao la 6,000 tangu ianze kushiriki Ligi Kuu ya Hispania, ilipoifunga Alaves mabao 3-0.

Bao la kwanza kati ya mawili aliyoyafunga kwenye mchezo huo ndilo lilifikisha idadi ya mabao 6000 kwa Barcelona tangu ianze kushiriki Ligi hiyo mwaka 1929 ikicheza michezo 2801.

Messi alifunga bao hilo dakika ya 64 kwa mpira wa adhabu uliopita juu ya ukuta wa Alaves, kabla ya mtokea benchi Philippe Coutinho kuongeza la pili dakika ya 83.

Wakati wengi wakiamini mchezo utamalizika kwa Barca kushinda mabao 2-0, Messi akafunga bao la tatu akionyesha uwezo mkubwa kwani alituliza kifuasi mpira aliopewa na Luis Suarez, akaumiliki na kuwapiga chenga mabeki wawili, akampiga chenga kipa na kuujaza mpira wavuni.

Mesi amezidi kujiwekea rekodi katika Ligi Kuu Hispania na kwa klabu yake kwani ndiye mchezaji aliyeifungia Barca mabao mengi zaidi, pia Februari 1, 2009 aliifungia bao la 5,000 walipocheza na Racing Santander.

Katika historia ya Ligi Kuu Hispania ni Real Madrid pekee ambayo imefunga mabao zaidi ya 6,000, ikiwa imefunga mabao  6,041 katika mechi 2,800.

Aidha mabao hayo yamemuwezesha Messi kufikisha mabao 385 katika La Liga yote akiwa ameifungia Barcelona.

Kati ya mabao hayo 6,000 ya Barca, walioandika rekodi kwa ufungaji ni, Manuel Parera aliyefunga bao la kwanza la timu hiyo katika Ligi mwaka 1929, Marco Aurelio akaifungia bao la 1,000 mwaka 1950 Pedro Zaballa akafunga bao la 2,000, mwaka 1964, bao la 3,000 likafungwa na Quini mwaka 1982, bao la 4,000 likafungwa na Guillermo Amor mwaka 1996 bao la 5,000, Lionel Messi mwaka 2009 bao la 6,000, Lionel Messi, Agosti 18, 2018.