Messi aiongoza Barca kulipa kisasi kwa Levante

Muktasari:

  • Barcelona imelipiza kisasi cha kufungwa mabao 5-4 na Levante katika mechi ya La Liga msimu uliopita, baada ya jana kuibamiza kwa mabao 5-0, nahodha wa timu hiyo Lionel Messi, akifunga mabao matatu ‘hat trick’ na kupika mawili, ushindi unaowaweka kileleni kwa pointi tatu zaidi.

Barcelona, Hispania. Nahodha wa Barcelona, Lionel Messi, jana usiku aliwapa furaha mashabiki wa timu hiyo baada ya kufunga mabao matatu ‘hat trick’ na kupika mengine mawili katika ushindi wa ugenini wa 5-0 dhidi ya Levante.

Ushindi huo ulikuwa wa kulipa kisasi kwani ni timu hiyo ndiyo iliyowatibulia mkakati wa kumaliza bila kupoteza mchezo wowote katika msimu uliopita ilipowafunga mabao 5-4, hivyo Barcelona jana waliingia uwanjani wakidhamiria kulipa kisasi na wakafanikiwa.

Levante ilipata pigo katika dakika ya 76 baada ya mlinzi wake Erick Cabaco kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumchezea vibaya winga Ousmane Dembele.

Hata hivyo Barcelona walilazimika kuvuja jasho kupata ushindi huo kwani hadi dakika 35 timu hizo zilikuwa 0-0, ndipo Messi akafanya vitu vyake kwa kuwalamba chenga mabeki watatu na kupiga krosi iliyomkuta Luis Suárez na kuuzamisha wavuni kirahisi.

Baada ya kuingia kwa bao hilo Levante walikuja juu wakitaka kusawazisha bila mafanikio na Messi tena aliwapa maumivu kwa kufunga bao la pili katika dakika ya 43 hivyo Barca kwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao 2-0.

Messi aliendeleza ubabe wake kwa kufunga mabao mengine mawili katika kipindi cha pili dakika ya 47 na 60 kabla ya kumtengenezea beki Gerald Piqué aliyefunga bao la mwisho dakika ya 88.

Kwa hat trick hiyo Messi amefikisha mabao 50 aliyoyafunga kwa klabu na timu ya Taifa ya Argentina kwa mwaka huu 2018 pekee.