Messi apiga bao 100, akiiua Chelsea

Muktasari:

  • Ni wachezaji wawili tu waliofunga mabao 100 katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya

Barcelona, Hispania. Lionel Messi ameungana na Cristiano Ronaldo kwa kufikisha mabao 100 katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kufunga magoli mawili na kuiongoza Barcelona kuichapa Chelsea na kufuzu kwa mara 11 kwa robo fainali ya mashindano hayo usiku wa kuamkia leo Alhamisi.

Messi pia alitegeneza bao la Ousmane Dembele katika ushindi wao wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Camp Nou, pia Messi ndiye aliyeifungia Barcelona bao la kusawazisha katika mchezo wa kwanza uliofanyika London na kumalizika kwa sare 1-1.

Messi alimpiga tobo mara mbili kipa Thibaut Courtois akiwa katika kona mbaya kabisa pembeni mwa uwanja. Alifunga bao la kwanza katika dakika tatu na kuongeza bao tatu kwa Barcelona katika dakika 63.

Ronaldo kwa sasa anashikiria rekodi kwa kufunga mabao 117 akiwa ni mchezaji pekee aliyeweka rekodi hiyo katika mashindano hayo ya Ulaya. Messi amefikisha mabao 100, baada ya kucheza mechi 123, huku nyota wa Real Madrid alifikia idadi hiyo baada ya kucheza mechi 144.

Lakini ubora wa nyota huyo wa Argentina ambaye amerejea baada ya kukosa mechi moja akisherekea kuzaliwa kwa mtoto wake wa tatu wa kiume Jumamosi iliyopita, alionyesha wakati alipotegeneza bao la Dembele aliyefunga bao la kwanza tangu alipojiunga na Barcelona baada ya Messi kumpoka mpira Cesc Fabregas na kuwapita wachezajo wawili kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji.

Kocha wa Chelsea, Antonio Conte hakutaka kuwalaumu sana wachezaji wake waliopoteza nafasi kwa kugongesha mwamba mara nne, lakini alimwaga sifa kwa Messi.

"Nafikiri unapopata nafasi ya kumpa sifa mchezaji basi Messi, ni sahihi kuthaminika kama super, super, super zaidi," alisema Conte. "Tunazungumzia wachezaji wenye kitu cha ziada. Mchezaji bora duniani. Wachezaji wa aina hii wanazaliwa mara moja katika miaka 50."

Barcelona imeendeleza rekodi ya kutofungwa mechi 25 za Ligi ya Mabingwa kwenye Uwanja wa Camp Nou, mara ya mwisho kufungwa hapo ilikuwa 2013.

Barcelona sasa bado wanandoto ya kutwaa mataji matatu msimu huu, wakiongoza Ligi Kuu Hispania, wamefuzu kwa fainali ya Kombe la Mfalme na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Chelsea sasa wanatakiwa kuweka nguvu kupiganina kumaliza katika nne bora ya Ligi Kuu England ili kurudi katika Ligi ya Mabingwa msimu ujao kwa sasa wapo nafasi ya tano katika ligi.

Katika mchezo mwingine uliochezwa jana usiku ulishudia Bayern Munich ikishinda 3-1 dhidi ya Besiktas na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 8-1.