#WC2018: Messi ashikilia tiketi ya Nigeria

Muktasari:

  • Argentina na Nigeria zinavaana keshokutwa katika mchezo wa tatu kwa kila timu unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali.

Moscow, Russia. Nahodha Argentina Lionel Messi, ana tiketi ya Nigeria ‘Super Eagles’ ya kufuzu hatua ya mtoano katika Fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

Argentina na Nigeria zinavaana keshokutwa katika mchezo wa tatu kwa kila timu unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali.

Messi anayecheza Barcelona, ni mshambuliaji hatari anayepaswa kuchungwa katika mchezo huo.

Ingawa Nigeria imeishika pabaya Argentina, baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Iceland, matumaini ya Waafrika hao kusonga mbele yako mikononi mwa Messi.

Messi atacheza mchezo huo akitaka kuifuta rekodi ya mshambuliaji Ahmed Mussa wa Nigeria, aliyefunga mabao yote mawili dhidi ya Iceland.

Mchezo wa Jumanne utaamua hatima ya Messi kubaki Russia au kufungasha kirago mapema kabisa kurejea nyumbani Buenos Aires.

Argentina itacheza kwa tahadhari kubwa ikitaka kupata ushindi ambao utarejesha furaha kwa mashabiki wa nchi hiyo ambao wamekata tamaa.

Endapo Nigeria itaondolewa katika hatua ya makundi, itakuwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2002 katika fainali zilizochezwa Japan na Korea Kusini.

Argentina yenye pointi moja baada ya kutoka sare na Iceland, inatakiwa kushinda ili kusonga mbele katika fainali hizo, lakini ikifungwa au kutoka sare ya aina yoyote itakuwa imekata tiketi ya kurejea nyumbani.

Baada ya kuanza vibaya kwa kufungwa na Croatia mabao 2-0, Nigeria imejiweka katika nafasi nzuri kwenye kundi lake baada ya kuvuna pointi tatu na ipo nafasi ya pili. Croatia tayari ina pointi sita.

Argentina inayoburuza mkia katika kundi hilo, ina kibarua kigumu kupata pointi tatu mbele ya Nigeria katika mchezo wao utakaopigwa kwenye Uwanja wa St Petersburg.

Hata hivyo, ushindi wa Argentina utakuwa na manufaa kwa kutegemea matokeo ya mchezo kati ya Iceland na Croatia zinazotarajiwa kuumana mjini Rostov.

Iceland itacheza mchezo huo ikiwa na pointi moja na ikishinda itafikisha pointi nne ambapo itakuwa sawa na Argentina endapo itaifunga Nigeria, hivyo uwiano wa mabao utaamua timu ya kusonga mbele.

Kwa mfano Argentina ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Nigeria na Iceland ikaibuka na ushindi wa mabao 2-0, Argentina itasonga mbele kwa uwiano mzuri wa tofauti ya mabao.

Endapo Argentina itashinda mabao 2-0 na Iceland ikashinda bao 1-0, zote zitakuwa na pointi nne kila moja, hivyo uamuzi wa timu moja kusonga mbele utaamuliwa kwa tofauti ya mabao.

Lakini, timu hizo kila moja ikishinda bao 1-0, Argentina itatupwa nje katika fainali hizo kwa tofauti ya uwiano wa mabao ya kufungwa.

Mfumo wa 3-5-2 anaotumia kocha Gernot Rohr umekuwa na manufaa kwa Nigeria hasa baada ya kumuanzisha Mussa kucheza mbele dhidi ya Iceland.

“Nafurahishwa na timu hii inayoundwa na vijana ambao wako tayari kupambana. Nadhani kikosi hiki kitakuwa tayari kwa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022,” alisema kocha wa Nigeria.