Mexime bado yupo yupo sana Kagera Sugar

Muktasari:

Mexime ni moja ya makocha vijana Watanzania wanaofundisha Ligi Kuu

Kagera. Pamoja na kupata matokeo mabaya mfululizo kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime ameweka wazi kuwa hana mpango wowote wa kuachia ngazi.

 Timu hiyo ya mkoani Kagera, ipo nafasi ya 15 kwa pointi 14, huku ikiwa imefunga mabao tisa na kufungwa 17, na kushinda mechi mbili na kupoteza nane.

Kutokana na mwenendo usioridhisha wa Kagera Sugar 'Wanankurukumbi', mashabiki wa timu hiyo wameanza kumpa shindikizo kocha huyo wakimtaka aondoke.

Akizungumza hali hiyo, Mexime alisema hana mpango wa kujiuzuru kuifundisha timu hiyo kutokana na matokeo.

 Alisema kuwa licha ya matokeo waliyopata kwenye mechi zilizopita, anaamini mambo yatabadilika na timu itakaa vizuri mbeleni.

 "Hakuna kitu kama hicho, nijiuzuru kwa lipi? Huu ni mpira na ninaamini mambo yatakaa poa baadaye Ligi haijaisha hivyo tutulie hadi mwisho" alisema Mexime.

Aliongeza kuwa bado anaamini vijana watapambana na timu itamaliza Ligi ikiwa nafasi nzuri kwani timu zinatofautiana kidogo pointi.

Katika msimu uliopita,Kagera Sugar ilimaliza ikiwa nafasi ya tatu ikitanguliwa na Simba na Yanga  na Mexime kutwaa tuzo ya kocha bora wa msimu, lakini sasa inahaha kukwepa kushuka daraja.