Kocha Township Rollers aingiwa kiwewe soka la Yanga

Muktasari:

Kocha wa Township Rollers amewatahadharisha wachezaji wake kuwa wanaingia dimbani leo Jumanne kukutana na Yanga yenye uwezo wa kumiliki na kutawala mpira, huku wakiwa na uwezo mkubwa kushambulia.

Kocha wa Township Rollers, Nikla Kavazovic ameitahadharisha timu yake kuwa watambue kwamba wanakutana na klabu ngumu ya Yanga  ambayo ni miamba wa soka hapa nchini, huku akisisitiza kwamba kikosi chake kitawajibu kwa kushambulia wakati wote.

Kavazovic amesema hayo muda mfupi jana baada ya mazoezi ya timu yake kwenye Uwanja wa Taifa na akiweka bayana kwamba ni bahati mbaya au nzuri wanakutana na timu inayocheza soka sawa na kikosi chake.

Amesema Yanga ina kikosi kizuri ambacho kinajua kumiliki mpira, kutawala mpira na wanajua kutumia nafasi wakati wa kushambulia, lakini amesisitiza watahakikisha wanacheza kufa kupona ili kuwazuia.

Kocha huyo alisisitiza kwamba kikosi chake kipo fiti kuwavaa Yanga kwenye mchezo huo na mchezaji wao tegemeo Edwin Olerile ambaye alikuwa majeruhi atakuwapo uwanjani kusababisha mashabulizi.

Yanga na Rollers wanakutana kwenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijiji Dar es Salaam ambapo mgeni ramsi kwenye mchezo huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Dk Harrison Mwakyembe.