Miaka mitano ya nguvu maisha ya Cristiano Ronaldo

Muktasari:

  • Ikiwa ni moja taarifa mbaya zaidi katika masikio ya mashabiki wa Los Blancos, majira ya saa 12 na dakika 30, klabu ya Juventus, ilimtangaza Mreno Cristiano Ronaldo kuwa mchezaji wao mpya! Naam hiyo sio stori tena. Ameenda Turin.

HAKUNA safari isiyokuwa na mwisho. Hakuna sentensi isiyokuwa na kituo. Wanasema muda ni ukuta, huwezi shindana nao. Safari yake ya mafanikio na ufalme, katika viunga vya Jiji la Madrid, mji mkuu wa Hispania, umefika kikomo. Watamkumbuka!

Ikiwa ni moja taarifa mbaya zaidi katika masikio ya mashabiki wa Los Blancos, majira ya saa 12 na dakika 30, klabu ya Juventus, ilimtangaza Mreno Cristiano Ronaldo kuwa mchezaji wao mpya! Naam hiyo sio stori tena. Ameenda Turin.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni kwamba, wakala wa Ronaldo, Jorge Mendez, Rais wa Real Madrid, Fiorentino Perez na Mkurugenzi mtendaji wa Juventus, Giuseppe Marotta, walikubaliana kusaini mkataba wa miaka minne, uliohitimisha safari ya miaka tisa ya Ronaldo pale Santiago Bernabeu.

Ronaldo ambaye, alidokeza kuhusu kuondoka kwake nchini Hispania, baada ya kuiongoza, Los Blancos kutwaa taji la ligi ya mabingwa mara tatu, amekubali kwenda Turin, baada ya kukamilika kwa dili la pauni milioni 105. Inaitwa nguvu ya pesa.

Tuachane na hayo. Katika miaka tisa ya Ronaldo pale Santiago Bernabeu, kuna mambo mengi yaliyofanyika. Rekodi nyingi zilivunjwa na nyingine mpya kuwekwa, lakini Mwanaspoti inakuchambulia miaka mitano ya dhahabu katika maisha ya Ronaldo, tangu akiwa Old Trafford hadi Santiago Bernabue.

2008

Msimu wa 2007-08 ulimkuta Cristiano Ronaldo nchini England, katika dimba la Old Trafford m, akijiita shetani mwekundu wa Manchester United. Msimu huu, ukifungua dirisha katika maisha ya Ronaldo na kuruhusu mashabiki zake, wachungulie uwezo wake aliopewa na Mungu.

Katika msimu huu, Ronaldo alitupia mabao 42 kambani katika mechi 49, alizoingia dimbani. Mafanikio haya, yakamtambulisha Ronaldo katika uso wa Dunia ya soka. Kila mtu akamfahamu vizuri. Mabao yake yakampa Sir Alex Ferguson ubingwa wa ligi ya mabingwa na EPL.

 

2013

Mwaka 2013, ulikuwa mwaka wa Messi. Huu msimu Lionel Messi alikuwa hakamatiki, lakini bado Ronaldo hakumuacha apumue. CR7 alitupia mabao 59, katika mechi hamsini aliyocheza msimu mzima. Kila mtu akabaki akimpa saluti licha ya kushindwa kumpiku Messi katika tuzo za Ballon D'or.

2014

Baada ya kutupia mabao 59 katika mechi 50 za msimu wa 2013/14, Cristiano Ronaldo, aliendelea kukinukisha mwaka uliofuata (2014). Safari hii mabao yake yakaipatia Real Madrid mataji kadhaa.

 

 

Katika mechi 51, alizoingia uwanjani akiwa na uzi wa Real Madrid, Ronaldo alitupia mabao 56 kambani, n kuisadia Los Blancos kutwaa ubingwa wa Copa del Rey, UEFA Super Cup, Kombe la Dunia kwa vilabu (Club World Cup) na ubingwa wa 10 wa taji la ligi ya mabingwa maarufu kama 'El Decima'.

2016

Mwaka 2016, Ronaldo akaendeleza moto wake, akizama nyavuni mara 44 katika mechi 42. Madrid wakabeba ndoo ya ligi ya mabingwa Ulaya,  LaLiga, UEFA Super Cup na Kombe la Dunia kwa vilabu. Kama hiyo haitoshi, akaibeba Ureno na kuipa ubingwa wa kombe la Euro 2016, katika ardhi ya Ufaransa.

 

2017

Kubwa kuliko ni mwaka jana. Ronaldo na Kocha wake Zinedine Zidane wakaipatia Real Madrid taji lake la 13. Wakabeba ligi ya mabingwa mara tatu mfululizo. Yaani walipiga hat-trick na kuhakikisha UEFA wanarudi gareji kutengeneza kombe lingine baada ya kulibeba mazima.

Yote tisa. Mwaka jana akamfikia Messi katika idadi ya tuzo za Ballon D'or alipotangazwa mshindi wa tuzo hiyo huko Paris, akimbwaga Lionel Messi na Neymar dos Santos. Hata hivyo, hakuna aliyejua kuwa, hiyo ingekuwa tuzo yake ya mwisho ya Ballon D'or akiwa na jezi ya Real Madrid. Kwaheri 'el magnificent' Cristiano Ronaldo.