Mwadui yaondoka na pointi nne za Yanga, Simba

Muktasari:

  • Mwadui kwa sasa ipo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza michezo 17 ya Ligi Kuu

Kocha wa Mwadui FC, Ally Bizimungu ameweka rekodi ya kutokufungwa na Simba na Yanga msimu huu kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Mnyarwanda huyo tangu ametua Mwadui mwishoni mwa mwaka jana, hajapoteza mchezo wao dhidi ya vigogo hao wa soka nchini baada ya kutoka suluhu na Yanga kabla ya jana kulazimisha sare 2-2 na Simba.

Akizungumzia mchezo huo Bizimungu alisema Mwadui walikuwa washinde mapema, lakini makosa ya vijana wake na waamuzi ndio yaliwapa pointi moja.

 “Simba tumewazidi sana, sema tatizo vijana wangu walishindwa kutumia nafasi walizopata na waamuzi pia hawakuchezesha kwa haki, lakini tutapambana na mechi zinazofuata,”alisema Bizimungu.

Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma alisema kilichosababisha wanaambulia pointi moja katika mchezo huo ni uzembe wa mabeki wake.

 “Ni makosa ya kizembe kwa mabeki wangu lile bao lilikuwa dhaifu sana, lakini hatukati tamaa na siyo kila siku tushinde leo (jan) tumegawa, lakini mechi zijazo tutashinda, mashabiki watulie ubingwa upo palepale,” alisema  Mrundi huyo.