Mshambuliaji Mrundi atikisa Msimbazi

Muktasari:

  • Uongozi wa Simba unapanga kumsajili mshambuliaji kutoka Burundi hivyo kulazimika kuondoa nyota kadhaa ili aweze kusajili.

Dar es Salaam. Usajili wa mshambuliaji wa Burundi anayechezea Rayon Sports ya Rwanda, Shazil Naimana huenda ukawa kaa la moto kwa wachezaji watano wanaocheza nafasi tofauti katika kikosi cha Simba.

Rekodi zilizowekwa na mshambuliaji huyo kwenye Ligi Kuu ya Rwanda msimu uliomalizika zinaonekana kuishawishi Simba iliyoamua kumfungia kazi mchezaji huyo ikiamini atakuwa dawa ya tatizo la ubutu kwa idadi kubwa ya washambuliaji wake ambalo timu hiyo unahisi linaweza kuwagharimu katika mbio za ubingwa.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 mbali na kuiongoza Rayon Sports kutwaa taji la Ligi Kuu ya Rwanda msimu uliomalizika, kabla ya hapo alikuwa sehemu ya nyota walioiwezesha Vital'O kutwaa ubingwa wa Burundi kwa misimu miwili mfululizo sambamba na kutwaa Kombe la Chama cha Soka Burundi.

Uwezo wa mshambuliaji huyo katika kufumania nyavu ulimwezesha kuibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi katika Ligi Kuu ya Rwanda mara mbili huku akifanikiwa kutajwa kama mchezaji bora wa mechi mara mbili. 

Licha ya Simba kuwa ndio timu iliyofunga idadi kubwa ya mabao kwenye Ligi Kuu hadi sasa ambayo ni mabao 21, bado safu yake ya ushambuliaji imekuwa ikipoteza idadi kubwa ya nafasi za mabao ambazo timu hiyo imekuwa ikizitengeneza huku lawama zikiwaangukia zaidi John Bocco, Laudit Mavugo pamoja na Juma Luizio ambao mara kwa mara wamekuwa wakicheza namba tisa.

Naimana aliyefunga mabao 16 katika mechi 27 alizoichezea Rayon Sports msimu wa mwaka 2016/2017 pia anaweza kucheza nyuma ya mshambuliaji, nafasi ambayo imekuwa ikichezwa pia na Emmanuel Okwi, Muzamiru Yassin au Haruna Niyonzima.

Hata hivyo Okwi anaonekana kutokuwa kwenye presha kubwa na ujio wa mshambuliaji huyo kwani anabebwa na mabao yake nane aliyoifungia Simba kwenye ligi hadi sasa lakini pia anaweza kucheza kama namba tisa au kushambulia kutokea pembeni.

Kama Naimana atafanikiwa kuhamishia makali hayo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, huenda Bocco, Mavugo, Luizio, Muzamiru au Niyonzima wakajikuta wakisotea benchi kumpisha Mrundi huyo.

Ingawa Simba imeonekana kuwa kimya juu ya usajili wa Naimana mwenye kimo cha sentimita 165 na kilo 68, mmoja wa viongozi wa klabu hiyo alilithibitishia gazeti hili kwamba mazungumzo baina ya Simba na mshambuliaji huyo yapo katika hatua za mwisho.

"Bado kumsainisha tu mkataba lakini tumeshakamilisha makubaliano naye ila kuna mambo machache ambayo yamefanya hilo lichelewe ikiwemo kungojea dirisha la usajili lifunguliwe.

Usajili wake umetokana na mapendekezo ya benchi la ufundi hasa kocha Masoud Djuma ambaye anamfahamu kiundani baada kufanya naye kazi kwenye kikosi cha Rayon," alisema kiongozi huyo.

Hata hivyo huenda usajili wa Naimana ukaambatana na nyota wengine wachache kutokana na kauli ambayo meneja wa timu hiyo Richard Robert aliwahi kunukuliwa juu ya kuhusu mkakati wao wa usajili.

"Tumefanya usajili mzuri msimu huu. Usajili ambao kila nafasi kuna wachezaji wawili ambao wana uwezo. Hatutokuwa na usajili mkubwa kwenye dirisha dogo kama tuliofanya kwenye dirisha kubwa. Kama ni usajili bali ni kwa nafasi ndogo sana," alisema Robert