Msukuma awakosoa maprofesa walioandaa mdahalo wa uchumi

Friday November 9 2018

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mapendekezo ya mpango wa taifa wa maendeleo wa mwaka wa fedha 2019/20 jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku ‘Msukuma’ amewataka maprofesa wanapoandaa midahalo kama ule wa uchumi uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwaita watu wenye elimu ya darasa la saba kwa sababu wana akili za kuchambua kuliko wao wenye makaratasi

Msukuma alikuwa akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka wa fedha 2019/20 bungeni leo Ijumaa Novemba 9, 2018.

Amesema wakati unatangazwa mdahalo uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hakutoka nje na aliweka hadi televisheni jimboni kwake ili watu waone Serikali ilivyofanya kazi.

“Mimi nilidhani mtachambua na kuwaeleza Watanzania kwamba uchumi miaka mitatu tangu (Rais John) Magufuli aingie madarakani tumefanya hivi katika kitengo fulani tumefanya hivi kwenye dhahabu kwenye madini.”

“Badala yake mmeenda kuchambua hotuba za Rais Magufuli. Maana yake Rais Magufuli anafanya vizuri nyie wakubwa mmeshindwa kuwaelimisha watu wakajua tulipotoka na tulipo na kelele hizi zikaisha. Maprofesa mnaenda kuchambua hotuba za Rais zile zile ambazo anatueleza na tunampenda kwa sababu hiyo hiyo,” amesema.

Msukuma akawashauri maprofesa inapotokea midahalo kama hiyo wawakumbuke na wao wenye akili za darasa la saba kwa sababu wanajua kuliko za kwao za makaratasi.

Kuhusu kodi amesema Watanzania wanakubali kuwa lazima kulipa kodi lakini unapokaa Dodoma ikifika saa 5.00 usiku polisi wanazunguka katika makarandinga kukamata watu.

“Mimi ninajiuliza hizi hesabu wanazopiga wakuu wa mikoa na serikali inaruhusu karandinga zinazunguka kalaleni, wageni wanakuja hapa Serikali imehamia hapa. Unaweza kuja kumuona Waziri hapa unaambiwa usubiri hadi keshokutwa.”

“Unakaa hapa mchana kutwa baa hazifanyi kazi kuna tatizo gani? Nani amewaambia wakiingia saa 5 vyumbani wanalala? Kuna tatizo gani watu wakanywa bia wakachangia Taifa?”

“Watu wakiingia katika magesti watapewa risiti, tuache ukiritimba wa kuwalaza watu saa 5.00.”

Amehoji wana wasiwasi gani kwamba makundi ya majambazi yana nguvu kuliko polisi.

Ameshauri pia magari yaruhusiwe kutembea usiku na polisi wa usalama wa barabarani waongezwe.

Advertisement