Msuva: Mbao haitashuka daraja

Muktasari:

Mbao msimu uliopita iliweka rekodi yakucheza fainali ya Kombe la FA, lakini msimu mambo yamekuwa tofauti kwao

Mwanza. Mshambuliaji wa Mbao FC, James Msuva amekiri  Ligi Kuu ni  ngumu tofauti na matarajio yao yalivyokuwa na kusisitiza kwamba bado hawajakata tamaa na wataendelea kupambana hadi mwisho.

Mbao imekuwa na mwenendo mbaya katika Ligi Kuu msimu huu, imevuna pointi 19 na kukaa nafasi ya 12 baada ya kucheza mechi 21 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Msuva alisema hali ilivyo hivi sasa ni wazi mambo yamekuwa magumu tofauti na walivyotarajia na kusisitiza kuwa bado anaamini watafufuka na kufanya vizuri katika mechi zinazofuata.

“Ni kweli matokeo siyo mazuri na sisi kama wachezaji tunaendelea kupambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ili kunusurika kushuka daraja,” alisema Msuva.

Aliongeza kuwa matokeo waliliyoyapata wanashindwa kuelewa nini tatizo, kwani uwanjani wanacheza vizuri, lakini mwisho wanajikuta wakipoteza mechi.

“Niwaombe wadau na mashabiki wetu watulie wasiwe na wasiwasi, tutajitathimini na kurekebisha kasoro zilizojitokeza ili timu iweze kumaliza vyema ligi ikiwa nafasi nzuri,”alisema mshambuliaji huyo.