Muuaji wa Yanga aweka rekodi tamu Mbao FC

Muktasari:

Nyota huyo ameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa (U-20), Ngorongoro Heroes, ameifungia Mbao mabao tisa hadi sasa na kuingia kwenye orodha ya wachezaji watano waliofunga mabao mengi msimu huu.

Mwanza. Mshambuliaji wa Mbao FC, Habib Kyombo ameweka rekodi ya kucheza mechi nyingi katika klabu hiyo akiwa amecheza mechi 25 sawa na dakika 2,250.

Nyota huyo ameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa (U-20), Ngorongoro Heroes, ameifungia Mbao mabao tisa hadi sasa na kuingia kwenye orodha ya wachezaji watano waliofunga mabao mengi msimu huu.

Kyombo amecheza mechi hizo ikiwamo tatu za Kombe la FA, amefunga mabao matano pamoja na tisa ya Ligi Kuu yamemfanya kufikisha mabao 14.

Meneja wa klabu hiyo, Faraji Muya alisema kucheza mechi nyingi mchezaji huyo kumempandisha kiwango chake na kufikia hatua ya kuongoza mabao kikosini.

Alisema kuwa wao wanaona ni faraja kwa mchezaji wao kuona anapata mafanikio, kwani mbali na kupigania timu kupata matokeo mazuri, wanahitaji afanikiwe yeye binafsi.

Kyombo alisema juhudi na kujituma ndio siri ya mafanikio yake na kwamba ataendelea kupambana kuhakikisha anakuwa na namba ya kudumu kwenye timu.

“Ni kujituma na kutokata tamaa, nawashukuru benchi la ufundi wanaotambua umuhimu wangu na kunipa majukumu, nitaendelea kuonyesha uwezo,”alisema Kyombo.

Wachezaji wengine waliocheza mechi nyingi zaidi Mbao ni beki Yusuph Ndikumana aliyecheza mechi 23, ndani ya kikosi hicho msimu huu huku kipa Yvan Rugumandiye  akiwa amecheza michezo 18.