Tanesco yatoa sababu umeme kukatika Simba, Al Masry

Muktasari:

Simba sasa wanahitaji kushinda au kupata sare ya zaidi ya mabao 3-3 katika mchezo wa marudiano ili kusonga mbele

Dar es Salaam. Mvua kubwa kunyesha, taa kuzimika uwanjani na kusababisha mchezo kusimama kwa takribani dakika 10 ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika mechi ya jana baina ya Simba na Al Masry ya Misri.

Mvua kubwa iliyoanza kunyesha kuanzia dakika ya 78, na kusababisha mwamuzi wa mchezo huo, Thando Helpus kutoka Afrika Kusini, kulazimika kusimamisha mchezo.

Hata baada ya mchezo kuanza upya, haukuwa kwenye ubora wake kwa kuwa wachezaji walicheza katika mazingira magumu kutokana uwanja kujaa maji.

Akizungumza jana usiku, Ofisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania, Tanesco, Leyla Muhaji alisema kuwa kutokana na mvua kubwa kunyesha, imesababisha hitilafu katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

“Mvua hii imesababisha umeme kukatika maeneo mengi ya jiji, Magomeni, Mikocheni, Tabata, Kinyerezi, Kitunda, Pugu, Ilala, Temeke…

“Tunawasiliana na mkoa wa Temeke kufahamu nini hasa kimetokea kwa kuwa Uwanja wa Taifa unapata umeme maalumu,” alisema Muhaji.

Soka kwenye maji

Baada ya umeme kurejea kwa baadhi ya maeneo, wachezaji wa timu hizo walishindwa kuonyesha ufundi kwa kuwa taa za uwanjani hapo hazikuwa na mwanga wa kutosha na kusababisha mchezo huo kukosa ladha.

Pia uwanja ulikuwa umejaa maji, kiasi cha wachezaji kushindwa kupiga gonga zilizoonekana kipindi cha kwanza.

Tukio kama hilo liliwahi kutokea mwaka 2001 katika michuano ya Kombe la Washindi,  Simba iliifunga Ismailia ya Misri mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Uhuru (zamani Taifa), lakini baada ya dakika 45 kipindi cha kwanza mvua kubwa ilinyesha na kusababisha mchezo kuvunjika.

Mchezo huo uliporudiwa siku iliyofuata, Simba ilishinda bao 1-0, hivyo ilitolewa kwa kuwa ilitakiwa kushinda mabao 3-0 kutokana na kufungwa 2-0 katika mchezo wa kwanza mjini Cairo.

Pamoja na mvua kuharibu mchezo huo, tatizo la wachezaji kukosa umakini ni miongoni mwa sababu zilizochangia Simba kushindwa kupata matokeo katika mchezo huo.

Pia, uzembe wa mchezaji mmoja mmoja na wachezaji kukosa mbinu mbadala pia zilichangia Al Masry kupata sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba ilizinduka dakika 45 za kipindi cha pili kutengeneza mashambulizi mfululizo kupitia pembeni, lakini ilichelewa kwa kuwa Al Masry ilitumia mbinu ya kucheza mchezo wa kujilinda zaidi.

Bao la pili liliwatoa Simba mchezoni na kutoa nafasi kwa wapinzani wao kutawala eneo la kiungo lililoshindwa kuwa na muunganiko mzuri na safu ya ushambuliaji.

Wachezaji wa kiungo walishindwa kupenyeza mipira kwa washambuliaji waliokuwa wakiongozwa na Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na nahodha John Bocco kabla ya kutolewa na nafasi yake kuingia Laudit Mavugo.

Pamoja na Simba kuanza mchezo kwa kasi, kupata bao la mapema, lakini wageni walitumia vyema udhaifu wa Simba kufunga mabao mawili yaliyowamaliza kipindi cha kwanza.

Mabadiliko ya upangaji wa kikosi yaliyofanywa na kocha Mfaransa Pierre Lachantre yalichangia kuiweka Simba katika wakati mgumu.

Katika mabadiliko hayo Shomari Kapombe ambaye amekuwa akicheza beki wa kulia, alipangwa namba sita, James Kotei anayecheza kiungo mkabaji alitumika kama beki wa kati huku mshambuliaji Nicholas Gyan akicheza kama beki wa kulia.

Eneo la kiungo la Simba lilikuwa na wakati mgumu baada ya wapinzani wao kulidhibiti na kuwapa wakati mgumu akina Jonas Mkude .

Huku ikishangiliwa na kundi kubwa la mashabiki wa Yanga waliojitokeza uwanjani hapo, Al Masry ilitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza.

Kasi ya mchezo ilivyokuwa

Simba ilianza mchezo kwa kasi licha ya kuchukua tahadhari ya kuwasoma wapinzani wao na dakika ya tisa ilipata bao la kwanza lililofungwa na Bocco.

Bocco alifunga kwa mkwaju wa penalti baada ya beki Mohammed Koffi kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari, lakini bao hilo liliiamsha Al Masry ambayo ilicharuka na kushambulia lango la Simba kama nyuki.

Al Masry ilitumia dakika mbili kusawazisha bao hilo kupitia kwa mshambuliaji nyota Ahmed Gomaa aliyeunganisha vyema mpira krosi iliyopigwa kutoka kushoto na Islam Atta.

Al Masry iliendelea kupeleka mashambulizi langoni mwa Simba na kupata bao la pili lililofungwa na Ahmed Abdalraof kwa mkwaju wa penalti baada ya Kotei naye kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Simba ilisawazisha bao dakika 74 lililofungwa na Okwi. Mshambulaji huyo wa kimataifa wa Uganda, aliwafunga tela wachezaji wa Al Masry na kumwangusha na mwenyewe akauweka mpira kimiani na kufanya matokeo kuwa sare.

Timu hizo zitarudiana baada ya siku 10, na Simba inahitahi ushindi wa aina yoyote ifuzu hatua ya nyingine ya kusubiri mechi za kapu kwa timu zitakazoshuka kutoka Ligi ya Mabingwa na baadaye sasa kukata tiketi ya makundi.